Amerika yamshutumu Rais Museveni kunyanyasa Wine

Amerika yamshutumu Rais Museveni kunyanyasa Wine

Na DAVID VOSH AJUNA

KAMPALA, UGANDA

UBALOZI wa Amerika nchini Uganda, umekashifu vikali kuendelea kuhangaishwa kwa mwaniaji wa Urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, kwenye kampeni zake za uchaguzi mkuu ujao.

Wine amekuwa akikabiliwa vikali na maafisa wa usalama kwenye msafara wake wa kampeni ambao hutibuliwa na kuishia yeye na wafuasi wake kukamatwa na kuzuiliwa na polisi.

Kisa cha hivi punde ni cha Jumatano ambapo Wine alikamatwa akiwa kampeni katika Kisiwa cha Kalangala. Polisi waliojihami walimnyaka na kumrejesha nyumbani kwake Magere katika Wilaya ya Wakiso ili asiendelee na kampeni zake.

Kukamatwa kwa Wine kulijiri siku 15 pekee kabla ya Uganda kuingia debeni Januari 15, 2021.

“Tukio la Jumatano ambapo polisi walitumiwa kumkamata mwaniaji huyo wa upinzani na wafuasi wake ni ishara kubwa kwamba Uganda haina demokrasia. Inashangaza kwamba kampeni za Rais Museveni hazivurugwi ilhali upinzani unakandamizwa kutokana na amri ya serikali,” ikasema taarifa ya ubalozi huo kupitia ukumbi wa Twitter.

Kando na Wine, polisi wa Uganda pia wamekuwa wakiwahangaisha wanahabari, kuwakamata baadhi yao na kuharibu vifaa vyao vya kazi kwa kupasha umma kuhusu kampeni za Wine.

Kufikia Jumatano usiku, msemaji wa NUP, chama anachotumia Wine kuwania uchaguzi huo alidai kuwa baadhi ya wanachama waliokamatwa na kiongozi huyo bado walikuwa wakizuiliwa na polisi.

“Wanachama wetu ambao walikuwa na mheshimiwa Kyagulanyi eneo la Kalangala walitiwa pingu kisha kurundikwa pamoja kwenye malori ya jeshi. Mmoja wao Eddie Mutwe anashuku kuwa wanapelekwa katika kituo cha polisi cha Masaka Central,” akasema msemaji huyo Joel Ssenyonyi.

“Mheshimiwa Kyagulanyi yupo nyumbani kwake Magere lakini boma limezingirwa na wanajeshi wala hawezi kutoka,” akaongeza Ssenyonyi.

Wine naye jana alidai kuwa wanachama 90 wa NUP walionyakwa Jumatano wanaendelea kuzuiliwa na polisi.

Uhusiano kati ya wanahabari na upinzani kwa upande moja na maafisa wa usalama upande mwingine umekuwa mbaya wakati huu wa kampeni.

Serikali nayo imekuwa ikimlaumu Wine kwa kuandaa misururu ya kampeni inayohudhuriwa na halaiki ya watu hali inayokiuka masharti yaliyowekwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Upinzani hata hivyo, unadai kuwa masharti hayo yanatekelezwa kibaguzi kwa kuwa Rais Museveni mara nyingi amekuwa akihutubia umma bila kuzifuata kanuni hizo.

“Haya masharti ya kuzuia corona yanatumiwa tu na Rais Museveni kuvuruga kampeni za upinzani. Ni masikitiko makubwa polisi wanatumiwa kuhangaisha upinzani na chama tawala kupendelewa,” akasema Msemaji wa FDC Ibrahim Ssemujju katika kikao na wanahabari.

You can share this post!

Wakulima, wafugaji wataka usaidizi wa serikali

Cavani apigwa marufuku na kutozwa faini ya Sh14 milioni kwa...