Kimataifa

Amerika yataka Tanzania kuongezea upinzani ulinzi

November 3rd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, Tanzania

AMERIKA imelaani serikali ya Tanzania kwa kuwakamata viongozi wa upinzani walionaswa kwa madai ya kupanga kuzua fujo.

Balozi wa Amerika nchini Tanzania, Donald J. Wright, aliitaka serikali kuwapa ulinzi badala ya kuwahangaisha.

“Nahimiza serikali kuhakikisha usalama wa viongozi wa upinzani. Serikali pia iachilie huru viongozi wa upinzani pamoja na wafuasi wao,” akasema Wright.

Balozi huyo pia alitaka serikali ya Tanzania kuondoa vikwazo vya matumizi ya huduma za simu na Intaneti.

Balozi huyo alitoa wito huo saa chache baada ya maafisa wa polisi wa jijini Dar es salaam kuthibitisha kuwakamata viongozi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwemo mwenyekiti wake Freeman Mbowe, kwa madai ya kuwashawishi vijana kuandamana.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu jijini Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema viongozi wengine wa Chadema wanaozuiliwa ni aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaam Boniface Jacob.

Maandamano ya viongozi wa vyama vya upinzani yalikuwa yamepangwa kuanza jana ili kushinikiza kurudiwa kwa uchaguzi mkuu huku wakisema shughuli ya kupiga kura Jumatano iliyopita iligubikwa na visa tele vya udanganyifu.

Rais Magufuli aliyeibuka mshindi baada ya kupata asilimia 84.4 ya kura zilizopigwa kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), anatarajiwa kuapishwa Alhamisi, wiki hii.

Aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema, Tundu Lissu tayari amepinga vikali matokeo ya uchaguzi huo huku akiitaka jamii ya kimataifa kutotambua serikali ya Rais Magufuli.

Dkt Hussein Mwinyi jana aliapishwa kuwa rais wa Zanzibar katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.

Dkt Mwinyi ambaye hadi kuchaguliwa kwake alikuwa waziri wa Ulinzi wa Tanzania, alipata kura 380,000 (asilimia 76.27) na kumbwaga mshindani wake wa karibu Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT-Wazalendo na wawaniaji wengine wa vyama vya CUF na Chadema.

Wengine ambao wamewahi kuwa marais wa Zanzibar ni Abeid Amani Karume (1964-1972), Aboud Jumbe Mwinyi (1972-1984), Ali Hassan Mwinyi (1984-1985), Idris Abdulwakil Nombe (1985-1990), Salmin Amour Juma (1990-2000), Amani Abeid Karume, mwana wa rais wa kwanza (2000-2010) na Ali Mohamed Shein (2010 -2020).

Seif amepuuzilia mbali matokeo ya uchaguzi na amewataka wafuasi wake kuandamana.

Jumatatu, Mambosasa alisema polisi walipiga marufuku maandamano hayo, lakini viongozi wa Chadema walipuuza.