Amerika yatoa ahadi kusaidia Joho kufufua uchumi wa kaunti yake

Amerika yatoa ahadi kusaidia Joho kufufua uchumi wa kaunti yake

Na PHILIP MUYANGA

SERIKALI ya Amerika imejitolea kusaidia ufufuzi wa uchumi wa Kaunti ya Mombasa uliopata pigo kubwa kutokana na janga la corona.

Hayo yalibainika Jumatano baada ya Msimamizi wa Ubalozi wa Amerika nchini, Bw Eric Kneedler, kukutana na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho katika makao makuu ya kaunti hiyo.

Uchumi wa Mombasa uliathirika sana na janga la corona kwani kaunti hiyo ni miongoni mwa zile za Pwani zinazotegemea sana utalii.

Janga la corona liliathiri safari za kimataifa na biashara zinazotegemea sekta ya utalii.

Mbali na hayo, Amerika pia iliahidi kushirikiana na kaunti hiyo kuboresha usalama.

Sekta ya utalii awali ilikuwa pia imeathirika na mashambulio ya kigaidi yaliyofanya baadhi ya mataifa ya kigeni kuwaonya raia wao dhidi ya kuzuru nchini hadi sasa.

Akizungumza baada ya mkutano wao, Bw Joho aliomba wakazi wa Mombasa wajitokeze kwa wingi kupokea chanjo ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

Inatarajiwa kuwa shughuli za kawaida zitaruhusiwa kurudi ikiwemo kuondolewa kwa kafyu iwapo idadi kubwa ya wananchi watapokea chanjo.

Bw Joho aliondolea wakazi hofu kuwa chanjo hiyo ni hatari akisisitiza kuwa hii si mara ya kwanza chanjo kutolewa nchini.

“Mimi nimepokea chanjo sawa na wale wote wanaosimama hapa mbele yenu. Kama wewe hutaki chanjo kibinafsi, ipokee kwa manufaa ya kulinda familia na wapendwa wako,” akasema.

Wito wake uliungwa mkono na Bw Kneedler ambaye alisema wananchi watajisaidia sana pamoja na taifa zima iwapo watajitokeza kupokea chanjo.

Alisema Amerika italeta chanjo zaidi humu nchini na kuongeza kuwa chanjo zinazoletwa ni sawa na zile ambazo zinatolewa kwa Waamerika kwa hivyo ni salama.

You can share this post!

Kenya kuadhimisha Siku ya Utamaduni

Mwanamume aliyenyimwa kitambulisho kulipwa fidia