Kimataifa

Amerika yawafurusha raia 50 wa Haiti waliotoroka vita nchini kwao

April 19th, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

WASHINGTON DC, AMERIKA

AMERIKA imewafurusha raia 50 wa Haiti ambao walihamia Washington kutokana na mapigano makali yanayoendelea Port-au-Prince.

Msemaji wa Wizara ya Usalama wa mambo ya ndani Amerika, alisema sera ya taifa lake haiwaruhusu watu ambao si raia na wasio na msingi wa kisheria kusalia nchini humo.

Afisa wa masuala ya uhamiaji nchini Haiti alisema kwamba jumla ya raia wake 52 waliwasili katika uwanja wa ndege wa mji wa Cap-Haitien Alhamisi.

Kwingineko huko Sudan, jumla ya watu 391 wamekufa kutokana na kipindupindu na homa ya dengue tangu mapigano yazuke nchini humo.

Tangazo hilo lilitolewa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

“Takriban visa 11,000 vya kipindupindu vimerekodiwa, vikiwemo vifo 325 katika majimbo 12, huku visa vya homa ya dengue vikifikia 9,000, vikiwemo vifo 66,” Waziri wa Afya wa Sudan, Haitham Mohamed Ibrahim alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Waziri huyo pia alisema licha ya vita hivyo, Wizara ya Afya imeweka mikakati ya kutosha hasa katika majimbo yaliyoathiriwa na kipindupindu ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Akizungumzia juhudi za wizara ya kutoa huduma za kimsingi za afya, waziri huyo alibainisha kuwa kutoa huduma za afya katika majimbo na mikoa yote ya Sudan ni suala wanalolipa kipaumbele.

Kwa mujibu wa waziri huyo, takriban tani 4,000 za dawa za kuokoa maisha, zikiwemo dawa za kuwekwa kwenye mishipa, figo na saratani, na zile zinazotumika kwa maabara za matibabu, zimesambazwa katika majimbo mbalimbali.

Alifichua kuwa Wizara ya Fedha pia imetenga Sh3 trilioni ili kusaidia katika ununuzi wa vifaa vya matibabu.

Tangu vita vilipozuka kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (Saf) na Vikosi vya RSF mnamo Aprili 15, 2023, sekta ya afya nchini humo imekumbwa na matatizo kadhaa.

Kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (Ocha), watu 14,790 wameuawa na wengine milioni 8.2 wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mzozo huo kuzuka.