Kimataifa

Amerika yawawekea vikwazo wafadhili wa Al-Shabaab

March 12th, 2024 1 min read

NA REUTERS

WASHINGTON D.C., AMERIKA

WIZARA ya Fedha nchini Amerika, Jumatatu ilitangaza kuwawekea vikwazo watu na taasisi ilizozitaja kuwa sehemu ya mtandao ambao umekuwa ukitoa ufadhili wa kifedha kwa kundi la Al-Shabaab nchini Somalia.

Wizara hiyo ilisema mtandao huo pia umekuwa ukiendesha ulanguzi wa pesa ili kulisaidia kundi hilo kufadhili shughuli zake.

Viwazo hivyo vinalenga taasisi 16 na watu tofauti katika eneo la Upembe wa Afrika, Milki ya Kiarabu (UAE) na Cyprus.

Kwenye taarifa, Wizara hiyo ilisema itafunga akaunti za benki na mali yote ya taasisi na watu hao yaliyo nchini Amerika.

Mnamo Oktoba 2022, Amerika ilichukua hatua kama hiyo, ambapo iliwawekea vikwazo watu na taasisi kadhaa zilizohusishwa na tuhuma za kutoa ufadhili wa kifedha kwa kundi hilo.

Amerika ilisema kuwa kundi hilo huwa na mapato ya hadi Sh15 bilioni kwa mwaka.

Amerika imekuwa ikiliorodhesha kundi hilo kama la kigaidi.

Kundi hilo limekuwa likiendesha mashambulio dhidi ya serikali ya Somalia tangu 2006, likilenga kubuni himaya yake ya utawala.

Kundi hilo limekuwa likihusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

“Tishio la Al-Shabaab haliikabili Somalia pekee,” akaeleza msemaji wa Wizara hiyo, Matthew Miller, kwenye taarifa.

“Fedha inazopata Al-Shabaab huwa zinatumwa kwa makundi mengine yenye uhusiano na Al-Qaeda kote duniani. Fedha hizo huwa zinatumika katika kuendesha na kufadhilo vitendo vya kigaidi,” akaongeza.