Habari Mseto

Amerix awatia kiburi wanaume wa Tanzania ‘wasilipie’ mapenzi

January 11th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

MTAALAMU wa Afya ya Uzazi na Mvumishaji masuala ya afya njema ambaye ameibuka kuwa mtetezi wa maslahi ya wanaume maarufu Amerix, amewarushia chachawizo wanaume wa nchi ya Tanzania.

Amerix amesema wanaume wa Tanzania huwabembeleza wanawake na kuomba unyumba kwa kuwalipa.

Machapisho yake ya mfululizo katika mtandao wa kijamii wa X yameonekana kuwatweza wanawake na kuwakweza wanaume.

Kwenye chapisho la Jumatano Januari 10, 2024, Amerix aliwaita wanaume wa Tanzania masimpu wanaohangaika kupata mapenzi kwa kuwazawidi wanawake.

Yeye hutumia neno ‘simp’ kurejelea wanaume wenye hulka ya kuwafurahisha wanawake wanapotaka kitu kutoka kwao, akiashiria mwanaume sampuli hiyo ni mnyonge sana.

“Masimpu wa Tanzania wanaona vumbi kweli kweli. S***** haiombwi kwa zawadi, wewe ndiye zawadi, jenga fremu yako kwa uvumba na udi. Simpu na vumbi ni kama mapacha,” alisema Amerix na kuibua hisia mseto alimaanisha wanawake huwakubali wanaume bila hata kulipa.

Shabiki Hezbon aliyeshawishiwa na Amerix aliandika mtandaoni, “Kusimpu kutakulisha vumbi mpaka utashika adabu.”

Raia mmoja wa Tanzania kwenye mtandao wa kijamii wa X alijibu: “Hapa Dar es Salaam usiposimpu zigo utalionea kwenye video za Dayamondi.”

“Masimpu hufikiri kupeana zawadi ndiyo njia ya kupewa tendo la unyumba. Hawaelewi ya kwamba kuwa na fremu mwafaka ndiyo nguzo kwa wadada,” alisema Issah Khaleed.

Kupitia majukwaa yake mitandaoni, Amerix hupakia jumbe za kuwahamasisha wanaume wajiimarishe katika mawanda yote ya maisha, hususan afya na mahusiano, kupitia hash tag ya #MasculinitySaturday.

Kila wikendi maelfu ya wanaume hufuatilia mafunzo yake ambayo hatahivyo yamechukuliwa kuwa ya kuwadhalilisha wanawake.