Amevutia Wakenya kwa kuongea Kiswahili sanifu

Amevutia Wakenya kwa kuongea Kiswahili sanifu

Na CHRIS WAMALWA

DELAWARE, Amerika

MSIMAMIZI wa mji wa New Castle, jimbo la Delaware nchini Amerika, Bw Matthew Meyer, ameibuka kuwa kipenzi cha Wakenya wengi kwa sababu ya uwezo wake wa kuongea kwa Kiswahili.

Wakenya wanaoishi eneo hilo wamemtaja kiongozi huyo wanayemwita ‘Matt Mzungu’ kuwa aliye rahisi kufikiwa kwani hupokea simu zao wakati wowote, na huwa wanamwalika katika sherehe zao wanakozungumza Kiswahili.

“Tunamchukulia kama mmoja wetu kwa sababu ni mshirika wa karibu sana na jamii ya Wakenya. Anazungumza Kiswahili sanifu mno, hata huwezi kuamini,” akasema Bw Nick Nakitare, Mkenya anayeishi eneo la Bear, Delaware.

Kile ambacho wengi hawafahamu ni kuwa Meyer ana mizizi tele nchini Kenya.

“Nimewahi kuishi Kenya nikajua mengi kuhusu maisha ya Wakenya na tamaduni zao. Pia nina biashara nilizoanzisha Kenya na huwa ninasafiri huko mara kwa mara. Hapa Delaware, ninawafahamu Wakenya wengi na huwa tunajumuika pamoja. Wengi wao ni wafuasi wangu na marafiki,” akasema.

Bw Meyer ni mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya VituMob iliyo na makao makuu mtaani Hurlingham, Kaunti ya Nairobi.

Kampuni hiyo ni ya ununuzi wa bidhaa kupitia mtandaoni.

Awali katika mwaka wa 1995, alipokuwa mwanafunzi wa sheria nchini Kenya, alianzisha mradi wa Wikyo Akala, ambao ni wa utengenezaji viatu kwa kutumia magurudumu kuukuu ya magari.

Alianzisha mradi huo na rafiki yake, Benson Wikyo, ambao sasa umeajiri watu kadhaa mtaani Korogocho, Nairobi na viatu vinavyotengenezwa huuzwa katika nchi mbalimbali kimataifa.

Bw Meyer alizaliwa jijini Bay, Michigan akalelewa Wilmington, Delaware nchini Amerika.

Familia yake ilihama kutoka Michigan hadi Delaware alipokuwa mchanga. Alisoma katika Shule ya Wilmington Friends na Chuo Kikuu cha Brown.

Alipokuwa na umri wa miaka 21, Bw Meyer alipata ufadhili kutoka Chuo Kikuu cha Lawrence kuelekea Kenya kimasomo, ambapo alipelekwa Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Niliishi Kenya kwa miezi minne mara ya kwanza, na nilisafiri sana maeneo mbalimbali ya nchi. Niliwahi kuishi Kisii katika kijiji kilicho ndanindani kwa wiki moja, na Samburu kwa wiki mbili. Niliishi pia mtaani South B na Buruburu nilipokuwa nikifanya kazi Dandora na Mathare kwa hivyo nafahamu Kenya na Wakenya vyema sana,” akaeleza.

Kulingana naye, yale aliyoyapitia nchini humu yalimbadilishia maisha yake sana ikiwemo mtazamo wake wa ulimwengu.

“Kwa njia nyingi, nimefika mahali nilipo sasa kisiasa, kibiashara na uongozi wa kijamii kwa sababu ya yale niliyoyaona na kupitia nilipokuwa Kenya. Naweza kusema wazi kwamba maisha yangu yamekuwa bora kwa sababu ya yale nilipitia Kenya,” akasema katika mahojiano na Taifa Jumapili.

Alifichua kuwa, alipokuwa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, baadhi ya wahadhiri wake walikuwa Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana na Jaji wa Mahakama ya Juu Smokin Wanjala.

Bw Meyer alisema alipopewa nafasi kuja Kenya, alihitajika kuchagua kati ya uamuzi huo na kufanya kazi katika kampuni kubwa ya programu za kompyuta ya Oracle. Alichagua kuja Kenya na hajajutia uamuzi huo.

You can share this post!

Uhuru huenda apanga kumkweza Gideon kisiasa kurudisha mkono

DINI: Usikate tamaa, kipenga cha mwisho bado