Habari Mseto

Ameza sumu asubuhi asinyakwe na polisi

June 18th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MSHUKIWA wa wizi alijiua kwa kumeza sumu Jumanne, alipohofia kukamatwa na polisi.

Oscar Monda Omosa aliyekuwa na miaka 21 alifariki katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Nyamusi, wakati madaktari walikuwa wakijaribu kumhudumia baada ya kudaiwa kumeza dawa aina ya Acaricide.

Ilidaiwa kuwa polisi walikuwa wakimsaka kwa tuhuma kuwa alihusika katika wizi na kuvunja nyumba, walipomfumania nyumbani kwao katika kijiji cha Nyamusi, Nyamira Kaskazini saa kumi na moja alfajiri.

Kamanda wa polisi eneo hilo Timothy Muasya alisema kuwa mshukiwa alikuwa na dawa hiyo ya kuua wadudu tayari, na alipowaona polisi aliimeza mara moja.

Maafisa hao walimkimbiza hospitalini lakini juhudi za matabibu kumhudumia hazikuzaa matunda.

Kamanda huyo wa polisi alisema mshukiwa alikuwa amehusika katika wizi wa bidhaa ndogo ndogo za nyumba tu, wala hakukuwa na wizi mkubwa.

Kamishna wa kaunti Nyamira Amos Mariba alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la visa vya watu kujiua, kwa viwango ambavyo vinahofisha.

“Katika kipindi cha mwezi, tunashuhudia kati ya visa vitano na 10 vya watu kujiua, suala ambalo linahofisha,” akasema Bw Mariba.

“Visa vingi vimekuwa kutokana na matatizo ya kifamilia lakini hiki cha leo ni tofauti kwa kuwa mhusika alikuwa mshukiwa wa kosa la jinai, ambaye aliamua kufa badala ya kufikishwa kortini,” akasema.

Maiti ya marehemu ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Kaunti ya Nyamira, ambapo upasuaji unatarajiwa kufanywa.