Michezo

Amina atuliza joto la wanariadha kuhusu mbio za Diamond League

July 14th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAZIRI wa Michezo, Amina Mohamed, amewaondolea wanariadha wa Kenya hofu ya kutupwa nje ya mbio zijazo za Diamond League kwa kusisitiza kwamba Serikali na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) zinaendelea kushawishi balozi mbalimbali za nchi za Muungano wa Mataifa ya Bara Ulaya (EU) kuwapa wanariadha husika vibali vya kushiriki mashindano yatakayoandaliwa Ulaya mwezi Agosti.

Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyoachwa nje ya orodha ya nchi 15 za kwanza ambazo raia wao walipewa vibali vya kuzuru mataifa 26 ya bara Ulaya kuanzia Julai 1, 2020.

Watimkaji wa Kenya hawakujumuishwa pia katika ratiba iliyotolewa na waandalizi wa duru ya kwanza ya mbio za Diamond League zitakazofanyika jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14.

Wanariadha Joshua Cheptegei wa Uganda na Sifan Hassan wa Uholanzi, ambao ni wapinzani wakuu wa Wakenya katika mbio za mita 10,000 kwa upande wa wanaume na wanawake mtawalia, wamo katika ratiba hiyo.

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot, mfalme wa Jumuiya ya Madola Elijah Manangoi, Timothy Sein, Winny Chebet na Vincent Keter wanaonolewa kwa sasa na kocha Bernard Ouma, ni miongoni mwa Wakenya waliotazamiwa kunogesha kivumbi hicho cha Damond League.

Kwa mujibu wa Schengen News, ni mataifa matano pekee kutoka Afrika ambayo yamejumuishwa katika ‘orodha salama’ ya EU hadi kufikia sasa. Nchi hizo ambazo zimepiga hatua madhubuti katika vita vya kukabiliana na janga la corona ni pamoja na Uganda, Morocco, Algeria, Rwanda na Tunisia.

“Tumeshauriana na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) na kwa sasa tunajitahidi kuwasiliana na mabalozi wan chi husika za EU ili maamuzi hayo yabatilishwe. Wanariadha wetu wameteseka sana tangu shughuli zote za michezo zisitishwe kutokana na janga la corona,” akatanguliza Amina.

“Tusingependa kabisa waumie zaidi hata wakati huu ambapo majukwaa ya kushindana yamefunguliwa. Wameathirika sana kifedha na kwa upande wa makuzi ya kitaaluma,” akasema Rais wa AK, Jackson Tuwei kwa upande wake.

Mbali na Monaco, duru nyinginezo za Diamond League zilizotarajiwa kufanyika bara Ulaya msimu huu ni Stockholm (Uswidi) mnamo Agosti 23 na Brussels (Ubelgiji) mnamo Septemba 4.

Nyinginezo ni Roma/Naples (Italia) mnamo Septemba 17 na Gateshead (Uingereza) mnamo Septemba 26.

Tayari duru ya Paris iliyokuwa ifanyike Septemba 6 na mbio za Prefontaine Classic zilizoratibiwa kutifuliwa Septemba 20 zimefutiliwa mbali.