Michezo

Amina Mohamed chini ya shinikizo kuhusu Harambee Stars

September 13th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MAAFISA wa Uendelezaji Soka Mashinani katika Kaunti ya Murang’a (Murang’a Grassroots Soccer Development Team) wanamtaka Waziri wa Michezo na Turathi, Amina Mohamed atoe ruwaza rasmi ya kuimarisha kikosi cha Harambee Stars.

Wanalia kuwa ni aibu kubwa kuona mashabiki wa hapa nchini wakiwachambua wachezaji wa nje na timu zao kwa umakinifu lakini hata pengine golikipa wa timu ya taifa lao hawamjui.

Wamesema kuwa katika miji mingi ya hapa Kenya, huwa na mashabiki wa timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi za mataifa mbalimbali Ulaya.

Mashabiki hao hujumuika pamoja mara kwa mara kuchambua gozi linavyoendelezwa ughaibuni lakini ukiwauliza ratiba ya Harambee Stars, mara nyingi huwa hawaijui.

“Isieleweke eti hatupendi soka katika taifa hili na kwamba pengine sisi si wazalendo kwa kutojifahamisha na masuala ya Harambee Stars. Kinachochangia hali hii ni kule ‘kukosekana’ kwa mikakati ya kutupa mwongozo wa kuishabikia timu yetu,” ateta Simon Njoroge wa Murang’a Mjini, shabiki sugu wa klabu ya AFC Leopards.

Aongeza: “Waziri arejeshe uzalendo wetu katika timu yetu ya Harambee Stars. Tumechoka kushabikia timu za kigeni na ni juu yake kuimarisha kikosi chetu ili nasi tuwe na timu ya kushabikia katika vinyang’anyiro vya hadhi. Kwa sasa tumechochewa na hali duni yetu ya soka kujumuika na raia wa Ughaibuni kushabikia ligi zao; mimi nikiwajibikia ufuasi wa Arsenal.”

Wengine wamesema ni lazima Harambee Stars iimarike na iwe katika vinyang’anyiro muhimu duniani na kanda ya Afrika haraka “sio kwa kismati tu, lakini kwa uhakika”.

Akiongea na Taifa Leo katika mji wa Kigumo, mwenyekiti wa kundi hilo Bw Stephen Mahu alisema ni aibu kubwa kuwa hakuna juhudi zozote zinazotiliwa mkazo kuhakikisha mashabiki wa soka hapa nchini wamezinduliwa kikosi dhabiti cha kushabikia.

“Hatutaki kusema Bi Mohamed amelemewa na kazi yake lakini tathmini yetu kwa utendakazi wake ni kuona manufaa katika sera za michezo na hii itafanikishwa na kuona akizindua mikakati ya kutoa mielekeo mwafaka katika spoti,” akasema Bw Mahu.

Alisema kuwa hadi sasa Kenya haina jezi rasmi ya Harambee Stars ambayo imefanywa rasmi na serikali na hata hakuna mikakati ya kuingia kwa mikataba na wafadhili wa kuuza jezi hizo kwa mashabiki.

“Ukiulizwa jezi ya Harambee Stars ni gani, labda useme ni bendera ya Kenya, au utaje rangi zinazotumika sana na vyama vya siasa. Hakuna anayeshughulikia suala hilo katika wizara,” akasema.

Aidha, alisema serikali ilikosea kutoa hazina ya uendelezaji wa soka mashinani kwa wabunge ambapo kila mbunge anasimamia kitita cha Sh1 milioni.

“Badala yake, pesa hizi zingejumuishwa pamoja na ianze kituo cha kufundisha wanasoka chipukizi hapa nchini; ikiwezekana katika kila wilaya. Hali ilivyo kwa sasa ni kuwa wabunge wanatumia kitita hicho kwa utumbuizaji katika hafla za kisiasa ambapo timu huambiwa zishindane ili wageni waheshimiwa wafurahie,” akasema.