Kimataifa

Amisom waondoka uwanja wa michezo Somalia

August 29th, 2018 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MOGADISHU, SOMALIA

MAAFISA wa kijeshi wa Muungano wa Mataifa (UN) hatimaye Jumanne walivunja kambi yao katika uwanja wa kitaifa wa Somalia, wakitoa nafasi kwa shughuli za michezo kurejea uwanja huo tena baada ya miaka mingi.

Kulingana na ripoti za mashirika, kikosi cha AU Somalia (Amisom) kina wanajeshi 20,000 kwenye kambi tofauti za kijeshi, moja ya kambi hizo ikiwa hiyo ya uwanja huo, ulioko jiji kuu la Mogadishu ambapo wanajeshi wamekuwa tangu 2011.

Waziri wa ulinzi Somalia Hassan Ali alisema kuondoka kwa kikosi hicho humo sasa kutatoa nafasi kwa uwanja huo kufanyiwa marekebisho na shughuli za michezo kurejea tena.

“Tunashukuru Amisom kwa kuirejeshea uwanja serikali kwa kuwa watu wa Somalia wamekuwa wakitaka hivi kwa muda mrefu ili shughuli za michezo zirejee,” akasema Bw Ali.

Jumatatu usiku, Rais Mohamed Abdullahi wan chi hiyo alizuru uwanja huo na kusema kuwa serikali itaurejesha katika hali yake ya awali.

Mechi ya mwisho kuwahi kuchezewa uwanja huo ulio na ukubwa wa kukaliwa na watu 6,000 ilifanyika 2003, kulingana na tume ya micheo ya Mogadishu.

Maafisa wa Amisom waliwatimua wanamgambo wa Al Shabaab ambao walikuwa wamepiga kambi katika uwanja huo kwa miaka mitatu hadi 2011, na kuufanya kuwa kambi yao.