Dondoo

Amlima mwenzake aliyefichulia mume siri

May 5th, 2019 1 min read

Na NICHOLAS CHERUIYOT

Ainamoi, Kericho

MWANADADA wa hapa alimrukia na kumtandika mwenzake akimlaumu kwa kumweleza mumewe kuhusu mkopo aliochukua kutoka chama chao.

Kulingana na mdaku wetu, mwanadada ni mwanachama wa chama cha akina mama eneo hili. Chama hicho kimenawiri na kina hazina ambayo wanachama huchukua mkopo wanapotaka.

Siku ya tukio, mwanadada alijaza fomu za kuomba mkopo na wenzake wakamdhamini. Baada ya saa kadhaa, alipata mkopo wa Sh100,000 na akafurahi mno.

“Pesa zangu ni siri yangu. Bwanangu hatapata hata shilingi ng’o! Nitatumia vile ninataka,” mrembo alisema kwa maringo.

Hata hivyo, njiani akielekea nyumbani alikutana na mumewe ambaye alimwambia maneno yaliyomshangaza.

“Leo umechukua mkopo kutoka chama na lazima tugawe nusu kwa nusu la sivyo hautalala kwangu leo,” jamaa alinguruma akitoka mangweni.

“Nani kakupa uongo kama huo? Siwezi kuomba loni bila kibali chako maana wewe ni mume wangu mpendwa,” kipusa alijaribu kumhadaa mumewe akiwa ameingiwa na baridi.

Si kipochi chako kina shilingi laki moja? Mimi si mtu hivi hivi. Ninatumia huduma za mganga maarufu na kila wakati ninafuatilia pitapita zako kimiujiza,” jamaa alidai.

Mrembo aliona hali si hali na akapiga kona kuhepa kisha akaelekea kwa kinara wa chama.

Alipompata, alizua sokomoko moja kwa moja akimlaumu kwa kutoa siri zake.

“Wewe ni mwenyekiti wa aina gani? Naona wewe ni kinara wa kuvunja ndoa! Utajutia kumpa bwanangu siri za mkopo wangu,” mwanadada alisema akihema kwa kasi.

Wawili hao wakaanza kuvurutana na kuangushana huku wakipiga nduru hadi wakatenganishwa.