Kimataifa

Ampiga risasi mpenzi wake kwa kukoroma usingizini

March 21st, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

MWANAMKE kutoka jimbo la Florida, Amerika amefunguliwa mashtaka ya kujaribu kuua baada ya kumpiga mpenzi wake risasi walipokuwa wakibishana kuhusu hali yake ya kukoroma wakati analala.

Idara ya polisi Kaunti ya Brevard ilisema kuwa Lorie Morin, 47, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kujaribu kuua, baada ya kumpiga risasi mpenzi wake wa wiki tatu, kwa kuwa alikuwa akikoroma kwa sauti ya juu wakati wa kulala.

Polisi walifahamishwa kuhusu kisa hicho Jumatano wiki iliyopita, japo wote mshukiwa na mpenzi wake walikiri kuwa hakupiga risasi kwa kutaka ila ilikuwa kimakosa.

Baadaye polisi walibaini kuwa mwanamke huyo alichochewa kumpiga mpenziwe risasi na ugomvi uliokuwa ukiendelea baina yao, kuhusu hali ya mwanamume huyo kukoroma, kwa sauti kubwa sana.

Nakala za korti zinaonyesha kuwa mwanamume huyo alikuwa amemtembelea mshukiwa usiku huo, huku ijapokuwa Morin alitarajia angekuwa na usiku mtulivu, ukageuka kuwa wa kelele si haba, kufuatia hali yake ya kukoroma sana.

“Wote walikuwa wakinywa pombe kabla na wakati wa ugomvi baina yao. Ugomvi ulizidi hadi Morin akatoa bunduki na kumpiga risasi mdhulumiwa,” polisi wakasema.

Hata hivyo, mwanamume huyo hakujeruhiwa sana.

 

Imetayarishwa na PETER MBURU