Ampotosha Rais?

Ampotosha Rais?

Na JOSEPH WANGUI

UTENDAKAZI wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Kihara Kariuki umepigwa darubini baada ya serikali kupoteza msururu wa kesi zinazowasilishwa dhidi yake mahakamani.

Afisi hiyo pia imelaumiwa kwa kubuni vyeo ambavyo si vya kikatiba ili kumfurahisha Rais Uhuru Kenyatta huku serikali nayo ikiendelea kulemewa kortini tangu 2013 na kuongeza uhasama kati ya afisi ya Rais na idara ya mahakama.

Afisi ya Mwanasheria Mkuu ndiyo mtetezi wa serikali kuhusu maswala yote ya kisheria na inatekeleza majukumu yote ya kuhakikisha sheria inazingatiwa.

Mnamo Jumatano, Jaji wa Mahakama Kuu Anthony Mrima aliamua kuwa Rais alikosea kwa kubuni wadhifa wa Waziri Msaidizi huku pia ikisisitiza mawaziri ambao wanahudumu katika kipindi cha pili cha Jubilee baada ya kuteuliwa tena, walifaa kupigwa msasa na bunge.

Pia, Jaji Mrima alishikilia kwamba, ni haramu kwa mtu yeyote kuteuliwa kama Katibu katika wizara yoyote bila kutuma maombi ya kazi hiyo, kuhojiwa kisha jina lake lipendekezwe kwa Rais na Tume ya Kuwaajiri Wafanyakazi wa Umma (PSC) ndipo ateuliwe katika wadhifa huo.

Mwanasheria mkuu pia alipoteza kesi ambapo Rais Kenyatta alilaumiwa kwa kukataa kuwaapisha majaji 41 walioidhinishwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC). Mahakama iliamua mnamo Februari 6 kuwa, kuchelewesha kwa uteuzi huo kulikuwa kinyume cha sheria na kuamuru majaji hao waapishwe ndani ya siku 14.

“Baada ya JSC kufanya uamuzi, Rais hana mamlaka yoyote ya kuubatilisha au kukataa kuwateua majaji hao. Kisheria lazima awateue majaji hao waliopendekezwa kwake,” likasema jopo la majaji waliotoa uamuzi kwenye kesi hiyo.

Mahakama Kuu pia imewahi kutoa uamuzi unaopinga kuhamishwa kwa kiwanda cha nyama cha KMC kutoka kwa Wizara ya Kilimo hadi Wizara ya Ulinzi na kuiongezea madhila afisi ya mwanasheria mkuu iliyomshauri kuhusu suala hilo. Jaji Mrima alisema uamuzi wa Rais ulikiuka katiba na umma ulifaa kushirikishwa kabla amri hiyo kutolewa.

“Uamuzi wa kuhamisha majukumu kutoka wizara moja au nyingine unafaa kufuata mchakato wa kisheria na umma unafaa ushirikishwe,” akasema Jaji Mrima.

Serikali pia ilipoteza kesi ambapo Rais alipinga uteuzi wa Jaji Mohamed Warsame katika JSC mnamo 2018 na baadaye akaapishwa na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga.

Katika kesi ya Jaji Warsame, serikali ilikuwa imekataa kuchapisha jina lake kwenye gazeti rasmi la serikali ikishikilia kwamba, lazima apigwe msasa na bunge la kitaifa.

Kesi nyingine aliyoipoteza Bw Kariuki ni pale ambapo Jaji George Odunga alizima amri ya Rais Kenyatta ya kuamrisha operesheni iendeshwe dhidi ya wafanyabiashara wanaouza pombe haramu mnamo 2016.

Jaji Odunga alisema operesheni hiyo ilikuwa kinyume cha katiba kwa sababu Rais hakufuata utaratibu wa kisheria unaohitajika. Rais alikuwa amewaagiza Wabunge waendeleze operesheni hiyo katika maeneo yao kuwaokoa vijana waliozamia unywaji wa pombe hiyo. Korti pia ilifuta sheria mpya za kudhibiti uuzaji wa pombe zilizoanzishwa na Wizara ya Usalama wa ndani mnamo 2015.

Mnamo Disemba mwaka jana, mahakama kuu ilifutilia mbali uteuzi wa wenyekiti na wanachama wa bodi kadhaa za mashirika ya serikali, uteuzi uliofanywa na Rais Kenyatta mnamo 2016.

You can share this post!

UDA yapinga talaka

Madai ya hujuma huku BBI ikibadilishwa kisiri