Amri waliozua hofu kura zikijumlishwa Mavoko wakamatwe

Amri waliozua hofu kura zikijumlishwa Mavoko wakamatwe

NA SAMMY KIMATU

skimatu@ke.nationmedia.com

KAMANDA wa polisi kaunti ya Machakos, Bw Isa Mohamud ameamuru makamanda wa divisheni za polisi katika kaunti ndogo ya Mavoko kuanzisha uchunguzi na kuwakamata washukiwa waliodaiwa kusambaza jumbe za kutia hofu.

Aidha, Bw Mohamud, amekanusha madai kwamba masanduku sita yaliyopatikana katika kituo cha kuhesabia kura cha NITA kilichoko mkabala wa Barabara kuu ya Nairobi/Namanga, katika eneo bunge la Mavoko mnamo Alhamisi jioni yalikuwa sio ya Mavoko.

Isitoshe, Bw Mohamud aliondoka ofisini kwake mara moja madai hayo yalipoenea kote Machakos na kufika haraka katika kituo cha kujumlisha kura.

Alikuwa katika msafara wa magari ya ulinzi yakipia ving’ora kutoka afisi za kaunti hiyo kuelekea “kulinda eneo la tukio.” .

Akizungumza na wanahabari, Bw Mohammed alisema uvumi huo unaweza kuzua ghasia na kuathiri amani ya kawaida ndani ya kaunti hiyo ambayo alisema huwa na utulivu katika misimu yote ya uchaguzi.

“Inasikitisha sana kwa watu kudai kujumlisha kura kumesimama baada ya kukatizwa na maajenti wachache ambao walikasirishwa na ‘kuzuia’ masanduku sita ya kura yaliyokuwa yamejazwa karatasi za kupigia kura,” alisema.

Katika maelezo yake, kamanda huyo alisema atakayebainika kueneza uvumi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Alisisitiza kuwa Msimamizi wa Uchaguzi (R.O) Bi Jane Wasirwa alilindwa na vyombo vya usalama na yuko salama.

“Hakuna kinachopaswa kukuzuia wewe madam R.O kutekeleza majukumu yako kutokana na vitisho vya wahuni wachache. Ninawahakikishia kuwa tunao maafisa wa polisi wa kutosha na ni lazima nyote mjue kwamba kufuatia usalama wetu kuimarishwa, tutawajia washukiwa waliotaka kuhujumu na kulemaza mchakato wa kujumlisha kura,” akaonya.

Kamanda huyo alimwamuru Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Bi Nancy Njoki kuongoza, kuchunguza kupitia ofisi ya DCIO wake na kumkamata yeyote anayeshukiwa kuhusika na ‘uvumi huo usio na msingi’.

Baada ya hotuba yake, Bw Mohamud alisema atazuru vituo vyote vya kujumlisha kura katika kaunti ya Machakos ili kuangalia masuala ya usalama.

Eneo bunge la Mavoko lina wapiga kura 118, 180 waliosajiliwa kulingana na tovuti ya IEBC kuhusu uchaguzi mkuu wa 2017.

Kulingana na Bi Wasirwa, ingawa alionekana kushtushwa na matukio, eneo bunge hilo lina wadi nne.

Wadi hizo ni pamoja na Athi River, Muthwani, Kinanie na Mlolongo.

Wakati tukienda mitamboni, ujumlishaji wa kura ulikuwa ukiendelea kufuatia vitisho hivyo.

Taifa Leo ilibaini kuwa karatasi na masanduku ya kupigia kura yanayodaiwa kuwa ya ajabu yalikuwa ni rasmi ya kupigia kura kwenye eneo bunge la Makovo na hayakuwa na dosari yoyote.

Baada ya kura kujumlishwa, mbunge anayeshikilia nafasi hiyo Bw Patrick Makau King’ola alitangazwa kuwa mbunge mtarajiwa baada ya kuzoa kura 40,123 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Bw Anthony King’oo Ngunga (10,369) na Gilbert Mutua Maluki (10,283) miongoni mwa wawaniaji 12.

  • Tags

You can share this post!

Winga wa kupanda na kushuka Paul Were sasa mali ya Rayon...

Wainaina Anthony Njoroge amshukuru Mungu na wakazi wa Kieni

T L