Michezo

AMROUCHE: Kenya yakodolea macho marufuku kutoka kwa Fifa

May 18th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) linatarajiwa kuandaa kikao nchini Uswisi leo Jumatatu kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu Kenya ambayo imepuuza makataa yake kadhaa ya kulipa Adel Amrouche fidia ya Sh109 milioni.

Kocha huyo Mbelgiji mwenye asili ya Algeria, alishtaki Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kwa kumtimua akiwa bado na kandarasi na Kenya ya kunoa timu ya taifa ya wanaume almaarufu Harambee Stars.

Mbelgiji Amrouche alinukuliwa majuzi akisema alitumia mali yake yote kulipa wakili akitafuta haki baada ya kutemwa na Kenya kabla ya kandarasi yake kutamatika Agosti 2014.

Alishinda kesi dhidi ya FKF, ambayo mara kadhaa imekuwa ikiomba iongezwe muda wa kulipa deni hilo. Hata hivyo, makataa ya mwisho, ambayo Kenya imepewa na FIFA kuwa imelipa Amrouche ni kabla ya Mei 18, 2020.

Hakuna habari kuwa FKF imelipa chochote kwa hivyo adhabu ya kuondoa Kenya kushiriki mashindano ya FIFA inatarajiwa kutangazwa siku yoyote kuanzia Mei 18.

Kenya, Mali, Uganda na Rwanda ziko katika Kundi E kwenye mechi za raundi ya kwanza za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022. Marufuku kutoka kwa FIFA itaondoa Kenya katika kampeni ya kuwania tiketi ya kuwa nchini Qatar mwaka 2022.