Habari Mseto

Amrushia rafiki mafuta moto kulinda mkewe

October 11th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MWANAMUME ameshtakiwa kwa kumchoma rafiki ya mkewe kwa mafuta moto ya kupikia na kumsababishia majeraha ya mwili.

Mahakama iliambiwa kwamba Bw John Odondi alimrushia Bi Diana Odisa mafuta moto mwilini alipojaribu kumzuia kumpiga mkewe.

Ilidaiwa kwamba mlalamishi alikuwa ameenda kumsalimia rafiki yake katika eneo lake la kazi mwendo wa saa moja jioni mshtakiwa alipofika na kumtaka afunge biashara yake waende nyumbani.

Alipokawia kufunga biashara, Odondi alianza kumpiga na mlalamishi akaingilia kati kuwatenganisha. Hata hivyo, mshtakiwa alichukua sufuria iliyokuwa na mafuta yaliyokuwa yakichemka na kumrushia kisha akatoroka.

Stakabadhi za kesi zilionyesha kuwa kisa hicho kilitendeka Oktoba 5 2018 katika eneo la Kangemi Dairy jijini Nairobi.

Mlalamishi alipelekwa hospitali na mke wa mshtakiwa ambapo alitibiwa na kuripoti polisi. Odondi alikamatwa na kufunguliwa shtaka la kumshambulia Bi Odisa na kumjeruhi.

Mshtakiwa alikanusha shtaka mbele ya Hakimu Mkuu wa Kibera Joyce Gandani na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh30,000 na mdhamini wa kiasi sawa au Sh20,000 pesa taslimu.

Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Januari 28, 2019.