Habari Mseto

Amsamehe aliyemdunga kisu

January 9th, 2020 1 min read

Na STEVE NJUGUNA

POLISI ambaye alidungwa kisu na mpenzi wake mnamo Jumapili kutokana na mzozo wa kinyumbani, sasa anataka mashtaka dhidi ya mshukiwa kuondolewa kortini.

Kostebo Sharon Wamuyu alimwambia Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Nyahururu, Bi Judith Wanjala kuwa alitaka kuondoa shtaka kuhusu jaribio la mauaji dhidi ya Paul Okato.

Mshukiwa ameshtakiwa kuwa mnamo Januari 5 mwaka huu, alijaribu kumuua Bi Wamuyu kwa kumdunga kisu mara mbili.

Hata hivyo, Bi Wamuyu aliwashangaza wengi baada ya kuiomba mahakama kuondoa mashtaka dhidi ya mshtakiwa, akisema kuwa amemsamehe.

Mwathiriwa, ambaye alipata majeraha mabaya kifuani, anahudumu katika Kituo cha Polisi cha Nyahururu,

Licha ya hayo, hakimu alimwagiza Bw Polycarp Wandera, ambaye ni afisa wa kuchunguza tabia, kuandaa ripoti maalum kuhusu mienendo ya mshtakiwa.

Mahakama iliambiwa kwamba mshtakiwa alijaribu kujinyonga baada ya kumshambulia mwathiriwa.