Habari Mseto

Amuua mkewe kwa kununua viatu vya Krismasi bila kumjulisha

December 28th, 2018 1 min read

Na KNA

SHEREHE za Krisimasi ziligeuka kuwa mkasa kwa familia moja katika mtaa duni wa Mawingo, Kaunti ya Pokot Magharibi, baada ya mwanamume mmoja kumuua mkewe kufuatia mzozo wa viatu vya Krismasi.

Baada ya kufanya kitendo hicho, mshukiwa alienda mafichoni.

Mshukiwa alimlaumu marehemu kwa kununua viatu vya kuvalia wakati wa Krismasi bila kumfahamisha.

Kulingana na Tom Makuto, ambaye ni jirani, wawili hao walianza kugombana kuhusu viatu ambavyo marehemu alikuwa amenunua ili kuvivaa siku ya Krisimasi.

“Wawili hao wamekuwa wakigombana mara kwa mara, ila siku hiyo marehemu alikuwa amenunua viatu. Wakati mumewe alipofika asubuhi, siku ya Krismasi, alivaa viatu hivyo bila kumwambia mkewe na kurudi siku iliyofuata. Mkewe alijaribu kumuuliza kuhusu kitendo hicho ila akamgeukia na kumuua,” akasema Bw Makuto.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi katika eneo hilo Mathews Kuto alisema kwamba wameanza msako dhidi ya mshukiwa kwani alifanikiwa kutoroka.

Mwanaume huyo alitambuliwa kama Jimmy Njoroge. Majirani walisema kwamba wawili hao walikuwa wamegombana kabla ya tukio hilo. Marehemu alidungwa kifuani mara kadhaa kwa kisu.

Majirani walimkimbiza mwathiriwa hospitalini ila akafariki wakiwa njiani.

Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Kapenguria.