Habari Mseto

Amuua mkewe na kujitia kitanzi

August 28th, 2020 1 min read

NA Steve Njuguna

Mwanaume wa miaka 41 alimuua mke wake Jumapili na baadaye akajitia kitanzi eneo la Shamata Kaunti ya Nyandarua.

Mwanaume aliyetambulika kama Antony Ng’ang’a alimuua mkewe Jane Wairimu wa miaka 35 kwa kutumia kisu cha jikoni  na shoka kabla ya kujinyonga nje ya nyumba yao Kijiji cha Ex Ndeiya eneobunge la Ndaragwa.

Kulingana na mjombake Antony, Bw John Macharia, msichana wa miaka 14 wa wawili hao ndiye aliyempasha habari hizo alipopata mwili wa mamayake Jumatatu asubuhi ukikuwa umelala chumbani kwake.

“Msichana huyo aliniambia kwamba aliamka usiku  akapata taa ikiwa imewashwa na mlango ukiwa umefunguliwa,akazima taa ,akafunga mlango na akarudi kulala,”alisema.

Bw Macharia aliambia Taifa Leo kwamba alikimbia nyumbani kwa binamuye na kupata mwanamke huyo akiwa amelala chumbani chake cha kulala.

“Niliambia majirani na tukaanza kumtafuta ndipo tulipata mwili wake umeninginia kwenye mti mita chache kutoka nyumbani kwake,”alisema Bw Macharia.

TAFSIRI NA FAUSTINE NGILA