Kimataifa

Amuua mkewe wakisubiri kesi ya talaka nje ya mahakama

May 15th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka Marekani amekamatwa baada ya kudaiwa kumdunga mkewe raia wa Japan kisu hadi kufa nje ya mahama moja Jijini Tokyo, walipokuwa wakisubiri kikao cha kusikizwa kwa kesi ya talaka baina yao.

Mashirika ya habari nchini Japan yalimtaja mwanamume huyo kuwa wa miaka 32 na raia wa US, japo hayakutaja jina lake.

Wawili hao walikuwa karibu na sehemu ya ukaguzi wa kiusalama nje ya mahakama hiyo wakati anadaiwa kumvamia mwanamke huyo na kumdunga kisu shingoni.

Mwanamke huyo wa miaka 31 alikimbizwa hospitalini, ambapo alitangazwa kufa alipofika.

Iliripotiwa kuwa mwanamume huyo alikuwa na visu vitatu na polisi wanaamini alimvamia mwanamke huyo punde tu alipoingia katika jengo la mahakama.

Polisi, hata hivyo, walidinda kudhibitisha ripoti hizo. Lakini picha za mashirika ya habari zilionyesha mwanamume mwenye kipara akilala sakafun polisi wakimdhibiti, muda ambapo kisa hicho kilitokea.

Haifahamiki ikiwa aliumizwa wakati wa matukio hayo na muda ambao polisi walichukua kabla ya kumkamata, baada yake kumuua mwanamke huyo.