Ana kijichumba cha wafuasi kujitakasa

Ana kijichumba cha wafuasi kujitakasa

NA LEONARD ONYANGO

WASHIRIKI wa dhehebu la Yesu wa Tongaren wanaamini kuwa, nyumbani kwa kiongozi wao ni Jerusalem.

Jerusalem kuna nyumba saba na kila moja ina kazi yake.

Unapoingia kwenye lango kuu, nyumba ya kwanza kukutana nayo upande wa kulia ni kijumba cha utakaso kilicho na kuta za matope. Waumini wote wanaokuja Jerusalem ya Yesu wa Tongaren wanapitia katika kijumba hicho kutubu dhambi zao kabla ya kuingia kanisani.

“Katika Kitabu cha Kutoka 30:17-20, Mungu aliambia Musa kuweka maji kwenye hema ambapo watu walifaa kusafisha miguu yao kabla ya kuingia kwenye madhabahu. Sisi pia tunafuata agizo hilo,” anaeleza Yesu wa Tongaren.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, hakuna maji ndani ya kijumba hicho cha Yesu wa Tongaren. Lakini anajitetea kuwa maji ni Roho Mtakatifu na wala si maji haya ya kawaida.

Nyumba ya pili Jerusalem ni kanisa ambapo waumini huabudu kila Jumamosi na Jumapili.

Kuna vijumba vitatu vya kupikia (jiko). Kijumba cha kwanza hutumiwa kupika na waumini wa kike walio katika hedhi.

Kijumba hiki cha wanawake walio katika hedhi kina sakafu na kuta za matope na hakuna kiti ndani.
Wanawake walio katika hedhi huvalia mavazi ya rangi nyeusi.

Wanawake hao huketi nyuma ndani ya kanisa na wala hawaruhusiwi kusimama, kusalimia waumini wenzao au kusema chochote kanisani. Baada ya ibada, wao hujitenga na wenzao na kuelekea katika kijumba chao.

Tulipotembelea wanawake hao katika kijumba hicho kutaka kujua kwa nini hawatangamani na wenzao, walichomoa Biblia na kutusomea Kitabu cha Walawi 15:19 kinachosema: Mwanamke yeyote anapokuwa mwezini (hedhi), atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Mtu yeyote atakayemgusa mwanamke huyo atakuwa najisi mpaka jioni.”

Kijumba kingine hutumika kupikia chakula cha waumini.

Yesu wa Tongaren hupikiwa chakula chake katika kijumba tofauti. Ni mkewe tu, Malkia, na mmoja wa waumini Nabii au Malaika Asher wanaoruhusiwa kuingia jikoni humo na kumpikia Yesu wa Tongaren chakula. Tulipomuuliza Nabii Asher (muumini wa kike) aliteuliwa vipi kuwa mmoja wa wapishi, Yesu wa Tongaren alisema aliteuliwa na Mungu kupitia ndoto na maono.

Kijumba kingine ni kile hutumiwa na watu wanaofunga kula. Nyumba inayoonekana kubwa ndiyo hutumiwa kulala na Yesu wa Tongaren pamoja na familia yake.

Yesu wa Tongaren ana watoto wanane – kifungua mimba wake anasoma katika chuo kimoja katika Kaunti ya Kiambu huku msichana anayemfuata akitarajiwa kujiunga na chuo baada ya kufanya vyema katika Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE).

  • Tags

You can share this post!

Ndani ya himaya ya ‘Yesu wa Tongaren’

Bungoma imegeuka mbingu yenye mungu, manabii na Yesu

T L