Makala

ANA KWA ANA: Afichua mambo mazito

July 19th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

MWANAMUZIKI maarufu wa injili hapa nchini Solomon Mkubwa, juzi katika mahojiano alifunguka mengi kuhusu maisha yake, uraia wake, kanisa lake jipya aliloanzisha na jinsi alivyokumbana na uchawi.

Stori yenyewe hii hapa:

Hebu waweke watu sawa, hivi wewe ni Mkenya?

Mkubwa: Mimi ni Mkenya Mkongomani ikiwa na maana kuwa naishi Kenya, tunayapitia pamoja, tunakula sukumawiki sote, maisha yanaendelea.

Umeishi Kenya kwa muda gani?

Mkubwa: Sasa hivi naingia mwaka wa 14.

Kilichokukwamisha Kenya ni nini hasa?

Mkubwa: Sijakwama Kenya, kazi ndiyo iliyonileta huku. Kisha nikapata kibali na ni kibali hicho kimenifanya kukaa na kuoa huku na kupata watoto wawili.

Kwa hiyo nyumbani Congo huna mke mwingine?

Mkubwa: (Akicheka) Nina mke mmoja Betty ambaye ni Mkenya. Sisi ni Wakristo, tumeokoka.

Ni kitu kipi kilichokuvutia kuoa Kenya?

Mkubwa: Sababu niliona maji ya mbali hayakati kiu. Na pia unakutana na yule mnaendana. Kuoana hauangalii tu uzuri. Unaangalia ikiwa huyu mtu tutafika naye mbali, atanipigisha hatua. Lakini pia mke wangu alifikia masharti yangu ninayozingatia nikimpenda demu. Mwanzo simpendi mwanamke anayeongea sana. Pili simpendi mwanamke mguu moto na ya tatu ni mwonekano mzuri.

Umesema kazi ndiyo ilikuleta Kenya, ipi hiyo?

Mkubwa: Nilialikwa Kenya na marehemu dadangu Angela Chibalonza kimuziki. Niliishi naye na mumewe kwa miaka mitatu na nusu toka 2003 kabla ya kifo chake. Alipotuacha ndio kipindi nilikuwa narekodi wimbo wa Mungu Mwenye Nguvu.

Kifo chake Chibalonza ulikipokeaje?

Mkubwa: Taarifa za tanzia nilizipokea nikiwa Kampala narekodi albamu iliyojumulisha wimbo huo Mungu Mwenye Nguvu. Tulikuwa tumeachana baada ya kupiga shoo Mombasa Jumatatu. Jumanne nikasafiri zangu Kampala kurekodi na Jumamosi ya hiyo wiki akatuacha. Nilishtuka vibaya sana sababu ni kitu ambacho sikuwa natarajia kwamba kinaweza kutokea kwa staili hiyo (ajali mbaya ya barabarani). Wajua kuna vifo vingine unaona mtu kaugua kwa muda mrefu sana unaona heri apumzike. Huyu alikuwa ndio anaanza kazi lakini ikatokea tu pap!

Ni nini kiliufanyikia mkono wako wa kushoto (uliokatwa)

Mkubwa: Mpango wa kando wa babangu alinitupia uchawi nikiwa na umri wa miaka 12. Nimetokea katika familia ya Kikristo lakini kipindi kile imani yetu haikuwa imara na ndio maana uchawi ukanipata. Babangu alikuwa ni mlevi na alikokuwa akienda kujiburudisha akaishia kukutana na huyo mwanamke. Baada ya kumpa mimba, aliikataa kwa sababu hakuwa amemwoa rasmi. Yule mwanamke alikuwa anatokea katika familia ya kishirikina na akasema atamfunza adabu kwa kuanza na watoto wake. Hapo siku moja nilianguka nikaumia mkono, ukapata uvimbe. Kwenda hospitalini hakuna ugonjwa ulioonekana. Niliteseka nao kwa miaka mitatu ukaoza na kilichobakia ni kukatwa tu hii ni baada ya hata kwenda kwa waganga pia. Na kipindi hicho pia tulimpoteza dadangu. Aliharisha wiki nzima akadondoka akafariki. Baada ya hapo ndipo tulijitambua tukarudi kwa Mungu wa kweli na ndipo wakashindwa.

Babako je?

Mkubwa: Alibadilika na kwa sasa ni mchungaji na mtumishi wa Mungu kule DRC japo wale watoto pacha (mmoja aliaga) hajawahi kuwakubali na huo ni uamuzi wake.

Mbali na kupoteza mkono wako, ulevi wa babako ulikuathiri vipi?

Mkubwa: Baba alikuwa anatusahau sana sababu ya ulevi wake na ikamlazimu mama kuanza kujitegemea ili kutulea. Shule tulifukuzwa sana. Kitu cha pekee na ambacho namheshimia baba ni kwamba pamoja na maisha yake ya ulevi, hakuwahi kumpiga mama hata siku moja. Mama angeteta, baba alimsikiza ila keshoye aliamka na kuendelea na yale yale. Nashukuru alibadilika.

Tukirudi kwenye usanii umefanya kolabo na Mr Seed, je, unaweza kufanya na Diamond Platnumz?

Mkubwa: Siwezi kufanya kolabo na msanii yeyote asiyekiri Yesu Kristo kuwa mkombozi wa maisha. Hata akija Diamond Platnumz akanitaka kolabo, sharti langu litakuwa hilo hilo amkiri Yesu Kristo na tutafanya kazi.

Umefungua kanisa, hili sio la kuwalia watu jasho lao jinsi ambavyo tumekuwa tukiona?

Mkubwa: Sio kila mtu yupo hivyo. Kama unamwambudu Mungu kwa kweli kama sisi, sadaka haiwezi kuwa chanzo. Kanisa letu tunamwabudu kwa ukweli na wala hakuna anayeshurutishwa kutoa sadaka. Tupo maeneo ya Kayole (Nairobi), tunawakaribisha watu waje waabudu na sisi na kama hawataridhishwa, basi wana uhuru wa kuondoka.