Makala

ANA KWA ANA: Beats kalikali zamgeuza kipenzi cha wanamuziki

August 16th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

VICTOR Mutungi ni mmoja kati ya wadau wakubwa wa muziki wa kisasa ndani ya +254.

Ukiwauliza mastaa wanaofanya vizuri kwa sasa kama vile Khaligraph Jones, Otile Brown, Arrow Bowy kati ya wengine huenda hawatamfahamu mara moja mpaka pale utakapowatajia jina Vicky Pon Dis.

Tulimshukia produsa huyu matata aliyehusika kwenye utengenezaji wa ‘hits’ kibao na kupiga naye stori.

Vicky Pon Dis bonge la lakabu mzee!

Vicky: Jina la kazi mzee. Limejifuma kabisa katika shughuli ninayoifanya. Lilitokana tu na utohozi wa lakabu yangu ya Kiingereza ‘Vicky on this’ nililoligeuza kuwa lafudhi ya Kijamaica.

Wewe ni kati ya maprodusa wanaoinukia na wanaotesa kwa sasa, shughuli hizi ulianza vipi?

Vicky: Nilianza kama mwanamuziki ila siku zote nilitamani kuwa produsa; sema kipindi hicho naanza kujihusisha na muziki sikuwa na mkwanja wa kununua vifaa vya utayarishaji muziki. Hivyo nikiwa mwanamuziki niliachia albamu mbili, nikapata vijisenti na kuanza kununua vifaa vya kutayarisha muziki.

Albamu mbili, acha wewe. Mbona hamna hata wimbo mmoja wako tunaoufahamu?

Vicky: (Akicheka) Albamu zote hizo zilikuwa nyimbo za kanisa ndio maana ziliishia tu kwa hadhira lengwa.

Baada ya kupata vifaa hivi, msanii wa kwanza uliyefanya kazi naye alikuwa nani na mlipatanaje?

Vicky: Msanii wa kwanza alikuwa Seroni, ni mshikaji wangu toka tukiwa kidato. Nilimtayarishia wimbo wake Shuga (2014) ambao kwa bahati nzuri uliishia kuwa ‘hit’ kubwa sana. Hapo sasa ndio wasanii wengine mastaa waliposikia zile biti, kina Otile Brown, Khaligraph Jones, Guardian Angel, Arrow Bowy, wakaanza kunitafuta wenyewe na taratibu nikaanza kujenga brandi yangu kwani kila niliyefanya naye, kazi ilishia kuwa kubwa. Hivyo kila aliyewauliza produsa aliyehusika, wakawa wanawatuma kwangu.

Msanii wa kwanza mkubwa kukufungulia uwanja akawa ni nani?

Vicky: Alikuwa Lady Bee. Kipindi hicho alikuwa ameokoka. Aliposikiza ile biti akaniomba tufanye kazi kadhaa naye na pia katika hilo ikanisaidia kunisukuma zaidi. Hapo ndipo akafuata Guardian Angel na wengine.

Jina lako lilipoanza kufahamika wengi walikutambua kama produsa wa injili?

Vicky: Hii ni kwa sababu kwa miaka miwili nilifanya kazi na wasanii wa injili hadi alipotokea Arrow Bowy na kuniomba tushirikiane. Alipenda biti zangu na kwa kuwa ni msanii wa Dancehall, aliamini itaingiana vyema na staili yake ya muziki. Toka hapo sasa ndio wenzake wa muziki wa densi wakaanza kuja.

Kwa sasa wewe ni miongoni mwa maprodusa wa kizazi kipya mnaofanya vizuri akiwemo Magix Enga. Ni kipi kinachokufanya wewe au nyie kuwa tofauti na maprodusa waliowatangulia?

Vicky: Wajua kila produsa anayo staili yake ambayo msanii anaweza kumfuata kutokana na aina ya wimbo anakusudia kurekodi. Kudumisha ule upekee wako ndio kunakupa utofauti. Kwa mfano mimi staili yangu ni kuunda biti za mdundo wa kasi.

Nimegundua pia wasanii wengi mastaa wamefanya kazi na wewe na bado wakamfuata Magix Enga ambaye tunaweza kusema anakupa ushindani mkubwa kwa sasa?

Vicky: Mwanzo yule ni mwanafunzi wangu, nimemfunza hii kazi kabla yake kuondoka. Sisi ni washikaji lakini pia na yeye anayo staili yake na ndio naamini wanakifuata wasanii hawa. Hii ndio sababu tumeweza wote kufanya kazi nao kutokana na upekee wetu.

Ila Magix yeye ni maarufu kukuliko?

Vicky: Kwa sababu yeye pia ni mwanamuziki, anaprodusi na kuimba hivyo huwezi kutegemea tukawa sawa. Mimi napenda kuwa nyuma ya pazia.

Msanii anapokufuata malipo huwa vipi?

Vicky: Hutegema na msanii na ukubwa wake ila malipo hayashuki Sh15,000. Haya ni malipo hasa ninayotoza msanii chipukizi.

Katika shughuli hizi ni changamoto zipi unazokutana nazo?

Vicky: Usumbufu hasa kutoka kwa wasanii chipukizi, wana presha sana. Hawajui kutulia. Mara nyingi ninaporekodi nao, mimi huwapa muda wa kunitafuta sababu usipofanya hivyo watakuchosha na simu za kila siku.

Umetayarisha zaidi ya nyimbo 100, ni nini kinachokufanya usirudie biti?

Vicky: Nafanya utafiti sana, nasikiza aina kibao za muziki lakini pia tusisahau mimi ni msanii. Nina ubunifu wangu hivyo natumia vigezo hivi kuwa tofauti katika kila kazi.

Kumekuwa na tetesi kwamba maprodusa wengi hamna uhalisia. Mnapenda kuiga biti za kazi nyinginezo?

Vicky: Ni kawaida ya shughuli zetu hizi hata video angalia nyingi huwa na ubunifu unaojirudia. Hili haliepukiki; kikubwa ni kuhakikisha unapoiga biti, na wewe unajitahidi kuiboresha zaidi.

Kwa wiki unaanda nyimbo ngapi?

Vicky: Hazipungui nyimbo kumi. Wasanii ni wengi sana wanaotokea kila leo kuja kurekodi.