Makala

ANA KWA ANA: DJ Mantix mbioni kujirejesha kwenye ramani

February 28th, 2020 2 min read

Na THOMAS MATIKO

MWONGO mmoja hivi uliopita, Barnabas Otieno almaarufu DJ Mantix, alikuwa gumzo sana hasa vilabuni na kwenye matatu kutokana na mix zake hatari.

Kila palipozuka mjadala wa MaDJ matata, jina lake halingekosekana, ila sio tena. Baada ya kupotea kwa muda, DJ Mantix akarejea na anajitahidi sana kujirejesha kwenye ramani.

Ulipotea mzee, siku hizi jina lako mtaani ni kama halina nguvu tena?

DJ Mantix: Kweli eeh! Ila nimerudi sasa na lengo langu ni kurejesha jina langu kwenye ramani kama zamani. Ukimya wangu kwa kweli ulisababishwa na kubanwa sana na majukumu ya kifamilia kiasi kwamba nikawa natumia muda mwingi kuwaangalia hadi nasahau kazi. Hufika muda ambapo familia hukuhitaji hata zaidi ya kazi yako na nafikiri ndio chanzo cha ukimya wangu.

Ulianza kama DJ wa muziki wa densi siku hizi toka urejee kwenye gemu nasikia umekuwa DJ wa injili vipi tena?

DJ Mantix: Hehehe! Mwanzo kabisa sijawahi kuwa DJ wa injili hizo ni stori zilizotungwa na mablogu baada yangu kufanya mix kadhaa za injili. Mimi bwana ni DJ wa aina yote ya muziki ilimuradi ni mzuri, sijui kubagua iwe ya dini au densi mimi nachapa tu. Na katika kazi hii lazima uwe mwepesi wa kwendana na trendi inayoshika kasi, kipindi hicho nilipobadilika na kuanza kufanya mix za injili, tasnia ya injili ilikuwa imeanza kuimarika na ikawa na mhemko wa aina yake na ndio maana nikajikuta nikifanya vile na mwisho wake ikavumishwa kwamba nimeokoka.

Hebu tuzungumzie suala lako la wewe kuingia mitini kipindi fulani ambacho ulikuwa ukifanya vizuri?

DJ Mantix: Wajua matatu ndizo zilizonipa umaarufu wangu na kunijengea brandi na hata nilipofanya mix za injili bado matatu zilizicheza. Halafu ghafla ndiko kukatokea zile sheria za (marehemu) Michuki zilizowekea vikwazo matatu kuwa na TV. Hatua hiyo iliniharibia kabisa brandi yangu kwa sababu hiyo ndiyo iliyokuwa tegemeo langu kubwa kujiuza, na hapo nikalazimika kugeukia biashara zingine ndogondogo ambazo hazikufanya vizuri. Ni kipindi hiki ambapo pia familia yangu ikawa inapanuka na kunipelekea kunibana na kunisababisha nipotee.

Katika karne ya sasa tunashuhudia baadhi ya ma-DJ siku hizi wakiangukia dili za kimatangazo ila sio wote, ni kipi wanachofanya tofauti?

DJ Mantix: Ni ishu nzima ya kuwa brandi. Unaweza ukakuta sio wakali vile inavyosawiriwa na wengi lakini uwezo wao wa kujijengea brandi ndio unaowawezesha kuonekana kuwa katika levo hizo. Unapokuwa DJ, ili kuwa na brandi lazima watu wakusikize na kukuona kila siku lau sivyo brandi yako itakuwa hafifu. Kwa mfano hao uliowataja, kila siku wanaonekana au kusikizwa. Kwa mfano DJ Mo anayo shoo kwenye NTV, vile vile DJ Sadic pale KTN, ni picha sawa na DJ Hassan aliye na shoo KBC. Naye DJ Mfalme kila siku anasikizwa kwenye shoo yake kwenye redio ya Capital FM. Unategemeaje wakose kuitiwa shoo wakati wao hao ndio kila siku wanaosikika na kuonekana?

Katika maisha yako ya kuwa DJ ni tukio lipi usiloweza kulisahau maishani?

DJ Mantix: Miezi kadhaa tulikwenda zetu Sudan Kusini kwa ajili ya kusaka riziki baada ya kutokewa na ofa tamu kutoka kwa promota mmoja. Tulikuwa kule kwa muda wa miezi mitatu tukifanya yetu haya ya u-DJ na mambo yalikuwa mazuri sana hadi mwezi wa mwisho yule promota alipoingia mitini na kutuacha kwenye mataa. Tulihangaika sana ukizingatia kwamba tulikuwa nchi ya wenyewe na tulipofanikiwa kurejea nyumbani hatimaye, tukakuta mambo mengi yamebadilika sana.

Una mke?

DJ Mantix: Ndio mzee na watoto pia.

Mkeo kazi yako hii anaichukuliaje?

DJ Mantix: Tumekuwa pamoja kwa miaka mingi sana hivyo ananielewa sana kwamba muda mwingi nakuwa sipo nyumbani nikihangaika kusaka riziki.