Makala

ANA KWA ANA: ‘Itanibidi niongeze dozi wakereke zaidi’

May 31st, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

RAPA Khaligraph Jones ameendelea kufanya vizuri kwenye tasnia ya burudani hapa nchini.

Hata hivyo siku za hivi karibuni amekuwa akitrendi kutokana na mabadiliko ya mwili wake toka alipoanza mazoezi ya vyuma.

Baadhi ya mashabiki wake wanaamini anatumia dawa za kututumua misuli na ndio sababu mwonekano wake umebadilika na sasa ni pandikizi la mtu.

Kwa mara nyingine safu hii ilimvizia na kuibuka na stori hii.

Toka mwaka umeanza ni kama vile unakesha gym?

Papa Jones: Zoezi ni lazima mzee. Watu wafanye mazoezi; sio kukonda tu. Ni muhimu kwa afya na maisha yetu.

Halafu hizi tetesi kwamba unatumia ‘steroids’ kutokana na mwonekano wa mwili wako kuvimba kwelikweli, vipi?

Papa Jones: Sijui matatizo ya watu ni nini, mimi nipo bize gym pamoja na muziki. Wanaochonga wacha watete. Naona nitazidi kuwakera tu. Itabidi niongeze dozi wakereke hata zaidi ili nao waingie gym au vipi hehehe!

Kuna kitu nimekigundua kwenye uzungumzaji wako, kuna wakati unazungumza vizuri halafu vipo vipindi unatia hiyo lafudhi ya Kimarekani?

Papa Jones: Hahaha! Si wajua tena mimi ni mwanaburudani mzee. Ila kuna usanii, na pia kuna mimi, hizi ndizo hulka zangu. Lafudhi ya Kimarekani imenikuta kutokana na aina ya muziki niusikizao.

Hivi ni kwa nini watu wana mtazamo kwamba wewe ni mtu mwenye kiburi na majivuno?

Papa Jones: Kwa wasio nifahamu. Nafikiri hamna mtu aliyetulia kunizidi mimi. Tumetangamana na wewe mara nyingi labda naweza nikakutumia kama shahidi. Ila lakini tena kama nilivyosema hapo awali, usisahau kwamba mimi ni mtumbuizaji na wakati mwingine nahitaji kuvalia hulka tofauti kwa sababu ya kazi niifanyayo.

Juzi mchizi wako Msupa S kazua kicheko kwa kuchana vitu visivyoeleweka. Nafikiri utakuwa umeicheki ile video. Ni kama vile ulimtosa baada ya kuahidi kumsaidia?

Papa Jones: Niliiona hehehe! Ninachompendea huyo binti ni ujasiri alionao na jinsi anavyojiamini.

Kuhusu ahadi yangu kwake, mipango ilibadilika. Yale mawazo na malengo niliyokuwa nayo ya kumkuza tulishindwa kuelewana. Ila hamna uhasama wowote kati yetu.

Tulianza vizuri, tukaachia ngoma Watajua Hawajui iliyofanya vizuri.

Wengi hawakuamini tulichokifanya kwa sababu ya kiwango cha Msupa S.

Lengo langu lilikuwa kumsaidia kufikia malengo yake kwenye muziki huu lakini kwa bahati mbaya hatungeweza kuendelea kwa sababu ambazo hazingeweza kuepukika.

Hivyo tukaachana kwa amani.

Alipoanza kutrendi nawe ukatokea na kufanya kazi naye, wapo wanaodai wewe ni mzee fursa, ulifanya vile kumtumia wala sio kumsaidia?

Papa Jones: Wa kusema watasema tu. Nawaachia wafasiri watakavyo. Ila acha nikuweke sawa. Mimi ni msanii mfanyibiashara na unapoiona fursa huiachi. Kama nilimtumia angekuwa analalama kwa sasa. Tulichokifanya kiliishia kutusaidia sote sema watu wanaona nilivyosaidika mimi ila hawaoni alichofaidi yeye.

Kuna kipindi umeulizwa kuhusu EX wako Ms Cashy ukajitia hamnazo, vipi mzee?

Papa Jones: Oya! Tafadhali tusirudi huko. Sina huo muda.

Hata baada yake kukuchana kwelikweli kwenye mahojiano unaona freshi kukausha?

Papa Jones: Mbona hatuelewani jomba? Unachoniuliza ni baadhi ya vitu visivyo na maana kwangu.

Mpenzio wa sasa huyo mjamzito siku zake zinakaribia, umejifunza na unajihisi vipi?

Papa Jones: Nazidi kujifunza mengi sababu hii itakuwa mara yangu ya kwanza kuwa mzazi. Nimeishi kutamani kuwa baba wa mtu na nashukuru Mungu ni mkubwa. Acha tusubiri.