Makala

ANA KWA ANA: ‘King Kaka na Naiboi wananisapoti sana’

September 20th, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

MIONGONI mwa wanamuziki chipukizi wanaoonyesha jitihada za kufa mtu ili kuweza kusimamisha brandi zao kwenye gemu humu nchini, yupo huyu kichuna Beryl Owano.

Hajakawia sana kwenye gemu ila kwa miaka mitatu au minne ambayo amekuwepo, mawimbi ya sauti yake yameweza kugonga kuta za Showbiz hapa nchini.

Mtoto wa kike anajiamini, bado muziki wake haujaanza kulipa ila anapania kupambana hadi mwisho. Hivi majuzi tumepiga stori na mtunzi huyu wa Kalipso.

Kipindi tunatafutana, uliniambia ulikuwa kwenye harakati za kushuti video mpya…

Owano: Eeeh! Ndio wimbo wangu mpya kabisa ‘Songa‘, video nimeshuti Jumatano wiki hii kisha baada ya kuhaririwa ndio nijue lini nitaachia. Natumai mashabiki wangu watapenda sababu kuna msanii Underscore nimemshirikisha pale, amekuwepo sana kwenye gemu sema hajulikani ila ana uwezo mkubwa.

Hili suala la msanii chipukizi kushirikisha msanii mkubwa hivi linasaidia?

Owano: Kwa asilimia fulani linasaidia kwanza kama ngoma ikiwa kali. Hebu kwa mfano waangalie Sol Generation leo wanajulikana sababu ya mchango wa Sauti Sol kwenye kazi zao.

Kwa nini usingelimshirikisha msanii mkubwa zaidi kwenye ‘Songa’?

Owano: Ndilo lililokuwa wazo langu la awali ila niliwafuata wasanii watano wakubwa, wanne wakiwa wa kiume na wote wakawa wananiyeyusha.

Walikuwa wanakuambiaje?

Owano: Aaah! Mtu hasemi, anakuzungusha tu badala ya kukuelezea ukweli kwamba hahisi kufanya kazi na wewe hivyo nikaona nisibembelezane nao na nikamsaka mbadala.

Au pengine walikuwa wanataka ulipie kolabo?

Owano: Wala, sababu hawa ni watu mara nyingi tunatoka nao, utatukuta kijiweni pamoja, ni watu ninaofahamiana nao.

Khuh! Kwa hiyo kama marafiki mbona waone ugumu?

Owano: Si wajua tena wasanii Wakenya tulivyo hatupendani ila tunaishi kwa kudanganyana. Tunasema tunapendana na ndani ya nafsi zetu hakuna anayetaka kumsaidia mwingine. Au mwingine anahisi kama akikusaidia atakujenga sana hivyo mimi kwa kuwa ni mtu mwenye uelewa, nilichunia tu.

Wewe ni msanii chipukizi na mdogo kiumri tuseme, unaweza kusema ni wasanii gani wakubwa waliokushika mkono bila ya kuwa na kinyongo?

Owano: Kusema kweli King Kaka na Naiboi hunisukuma sana mpaka wa leo. Ndio wasanii ambao hawajaonyesha kuchoka na ninachokifanya. Wananiamini sana na hilo nashukuru. Nimetamani kufanya nao kolabo ila wananiambia nizidi kupambana kwanza na siku ikifika tutashirikiana na hakika naamini ipo siku.

Miaka minne kwenye gemu, hivi muziki umeanza kukulipa?

Owano: Wala bado sababu sijaanza kupata shoo kivile na hata zile senti kidogo ninazopata zote nazirudisha kwenye muziki.

Sasa kama haulipi, mbona uendelee kupambana?

Owano: Mwanzo kaka kuna kitu kinachoitwa mapenzi, nafanya muziki sababu nina mapenzi nayo. Pili kuna suala la subra, siwezi kuanza jana nikategemea kufanikiwa kesho sema wapo wachache tulioanza nao ila nyota zao zikawang’aria mapema. Zile ni bahati. Lakini pia wengi wanaofanya vizuri sasa hivi walilazimika kusubiri kwa mfano Naiboi imemchukua miaka kuanza kupata hela. Wananiambia kuwa ili nianze kushuhudia malipo, nijipe miaka kama saba hivi kwanza na nipo tayari.

Kuna mtu atashindwa kuelewa basi kama hali ndio kama hii, ni nani anayefadhili muziki wako na video sababu hizi ni gharama?

Owano: Nina watu wanaoniamini katika kile ninachokifanya. Familia yangu na wadau wengine wa karibu. Lakini pia nina mambo yangu mengine ninayofanya kuingiza kipato.

Familia, hawajawahi kuchoka? Na mikakati hii mingine ni ipi au kuna sponsa?

Owano: Hahaha! Acha wewe. Kikweli huwezi kuitegemea familia kabisa au hata huyo sponsa ambaye sina. Mwenyewe pia najihangaikia. Ninaimba kwenye bendi za jijini Nairobi hivyo siwezi kukosa riziki sababu nachaji hela ndefu. Lakini pia natumika sana kama mwimbaji wa ‘back up’ vyote hivi vinaniingizia kipato.

Bado kwenye hili la familia nina mshikili?

Owano: Kwa nini tena? Naelewa unachokimaanisha ila wananisapoti sema babangu mzazi kidogo ndiye anayetamani kuona nikifanya kazi nyingine. Tayari nimeshajaribu ajira mara mbili kwenye kaunti ila mwisho wa siku zinaisha na ninajikuta nimerudi kwenye muziki na najua ipo siku sababu najiamini sana.