Makala

ANA KWA ANA: 'Kwangu mimi ndio kusema, ndio ndume'

June 21st, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

MWANAMUZIKI wa injili Kevin Bahati sio mgeni kwa wengi.

Alianza sanaa akiwa bwana mdogo mtulivu na mnyenyekevu, lakini sasa kabadilika.

Skendo zimekuwa sehemu ya maisha, muziki wake umeanza kudidimia huku yeye akionyesha kama vile kaanza kupoteza mwelekeo.

Tulikaa naye kijiweni kujaribu kumwelewa na mabadiliko haya ikiwemo maisha ya ndoa.

Majuzi tu, uliibuka na staili mpya ya nywele kwa kuweka rasta, baada ya kukashifiwa ukanyoa, maanake ilikuwa nini?

Bahati: Nilikuwa najaribu kitu tofauti sababu nimekuwa na staili hii (rasta fupi) kwa miaka sita iliyopita. Pia nilitaka kuwa na mwonekano wa kikomavu zaidi. Lakini ilibidi niziangushe sababu Wakenya wakizoea kitu ukibadilisha inakuwa ishu. Ila pia ilinisaidia kama kiki vile.

Mwonekano wa kikomavu eti eeh! Itakuwa ni suala la umri linakusumbua sababu hata mke wako alikushauri uzinyoe?

Bahati: Suala la umri kati ya mke wangu ambaye ni mkubwa wangu huwa halinisumbui kabisa. Tofauti yetu ni miaka mitatu tu sijui kwa nini watu huona ikiwa hoja kubwa sababu nyumbani mimi ndio kusema, mimi ndio ndume!

Uhusiano wako na mkeo ulianza kiutata sana, mliwahi kukana ukawa unasema yeye ni ‘prayer partner’.

Bahati: Eeeh! Kipindi hicho ilikuwa hivyo. Tulikuwa tunasaidiana kimaombi baadaye ndio mambo yakaja kubadilika na kutufikisha hapa.

Hivyo ni mke wako halali wa ndoa?

Bahati: Ndio!

Toka muoane wadau wamedai kuwa umekaliwa chapo. Wanahisi kuna baadhi ya maamuzi unalazimishiwa na Diana?

Bahati: Boma ni la mwanamke na endapo unataka maisha bila ‘stress’ nyumbani, basi jifanye zuzu na ukubali kukaliwa, utafurahia ndoa. Huu ni ushauri kwa wanaume kule nje.

Kunao pia wanaosema Diana alikufuata sababu ya hela zako?

Bahati: Watu wanaonifahamu mimi ni mgumu kwelikweli kwenye hela. Nafikiri Diana kajaribu sana kufaidi hela zangu, tena ni kwa sababu ni mke wangu.

Wakosoaji wako wanasema umepotoka kisanii, injili uliyotanguliza nayo sasa haipo?

Bahati: Naomba ieleweke kwamba mimi ni msanii wa injili na daima itasalia kuwa hivyo. Sio kwamba nimezamia masuala ya kidunia ila tuweni wakweli, baadhi ya mambo ninayojikuta nipo yanasababishwa na maisha yanavyokwenda. Sema dunia inapenda kutujaji sana.

Huu mzizi wa fitina kati yako na Mr Seed mtu ambaye umekuwa naye toka udogoni ni upi hasa? Nini kilitendeka kati yenu?

Bahati: Hamna kilichotendeka sema tulitofautiana tu kibiashara. Unapokuwa unafanya biashara lazima ukwende na uhalisia. Nilikuwa nimemsaini na sikuwa natengeneza faida, singejitia hamnazo kwamba kila kitu kipo shwari. Nilichokuwa nikifanya ni kumsapoti sababu wakati namchukua hakuwa anafanya vizuri kimuziki. Nilimsapoti kwa uwezo nilioweza sawia na nilivyosapoti wasanii wengine. Na unapomsaidia mtu, uamuzi wa kukushukuru au la ni wake. Alichokifanya ni kutunga stori ili iweze kutrendi na ndio sababu nilisalia kimya.

Toka mmetibuana umewahi kumtafuta mkazungumza?

Bahati: Sidhani kama tuna chuki. Mtu wa kumtafuta ni adui yako. Mimi nilimsaidia tu na wengine kibao, biashara ikawa haiendi sawa nikaamua kuachana nayo. Sasa kama wao hawakuichukulia poa, safi tu. Ndio maana baraka zangu zazidi.

Kwa hiyo hata mke wako hakuhusika sababu anadaiwa kuwa mchochezi kwenye ugomvi huu?

Bahati: Hamna! Diana mwanzo hayupo EMB Records. Sema wao walitaka tu kutrendi na jina lake sababu ana umaarufu mkubwa kuwazidi wao.

Halafu hii stori ya wewe kudaiwa na Mr Seed vipi?

Bahati: Yeye na wenzake ndio mwanzo ninawadai Sh6 milioni. Ni kama nilivyokuambia, walisaka stori ya kutrendi nayo wakaunga unga. Wako wapi sasa hivi? Wajifunze kushukuru wanaposaidiwa na watabarikiwa zaidi.

Drama zako zimekuwa kibao kiasi kwamba hata muziki ni kama umeusahau?

Bahati: Sio kweli, Ijapo sijaachia ngoma mpya kwa miezi mitatu. Nina albamu mpya ninayoshugulikia.

Halafu mpenzi wako wa zamani Yvette Obura kuchorwa ‘tattoo’ ya jina lako kifuani umechukulia vipi, Diana je?

Bahati: Sikutaka kujiingiza kabisa katika suala hilo wala kulijadili nisije nikaharibu uhusiano ulipo baina ya pande zote mke wangu na Yvette ambaye pia nimezaa naye. Nawaheshimu wanawake sababu ndio wamechangia mimi kufika hapa.

Ni kitu kipi hujawahi kufanya katika maisha yako ya kimaendeleo?

Bahati: Kuchukua mkopo, ila haimaanishi ni kitu kibaya. Nasema tu nimejaliwa kiasi kuwa ni mimi ndiye hukopeshana.

Ndoto kubwa uliyo nayo ni ipi?

Bahati: Kuwa bilionea kabla sijafikisha umri wa miaka 30.