Makala

ANA KWA ANA: Mmiliki wa Shirko Media aelezea safari yake katika fani ya burudani

August 24th, 2020 3 min read

Na FARHIYA HUSSEIN

ALIANZA kama mwanamuziki katika Kaunti ya Mombasa, akasafiri kuenda visiwani Zanzibar na akawa mtayarishaji bora zaidi ambaye anahusishwa pakubwa na kuanza kwa Yamoto Band na aina ya muziki wa Bongo Flava.

Miaka kadhaa baadaye, aliamua kurudi nyumbani – Kenya – na kukuza wasanii waliokuwa wanainukia.

Mmiliki wa Shirko Media anatoa maelezo katika mahojiano.

Unajulikana kama Shirko; kwa nini jina hilo?

SHIRKO: Jina langu ni Awadh Salim lakini nilipoanza safari yangu ya muziki nilikuwa shabiki wa mpira wa miguu ambapo jina Shirko linatoka kwa mchezaji wa Urusi anayejulikana kama Alexandra Shirko na hadi leo hii bado ni jina ambalo watu wananiita.

Kabla ya kuingia kwenye maisha ya kuwa mtengenezaji wa muziki, maisha yako yalikuwaje kama mwanamuziki?

SHIRKO: Nilianza muziki katika shule ya upili ambapo tulikuwa kikundi cha watu wawili wanaojulikana kama Lovely Brothers kabla ya kutengana. Tulikuwa tukienda kwa mashindano ya rap na kuimba. Mnamo mwaka 2003 tuliamua kuachia wimbo wetu wa kwanza tukitumia hela tulizoshinda kupitia kushiriki mashindano. Zama hizo tulikuwa tunaandika nyimbo zetu lakini hatukufanya hivyo kwa muda mrefu na ndoto zetu hazikutimia.

Ilikuwaje kutoka kwa mwanamuziki kwenda kuwa ‘Producer’ aliyejizolea sifa sana leo?

SHIRKO: Haikuwa kazi rahisi. Baada ya elimu ya shule ya upili, nilijiunga na chuo kikuu kusomea Uhandisi wa Kompyuta; kozi niliyofanya kwa mwaka mmoja tu. Wakati huo nikiwa chuo kikuu, kulikuwa na studio Mombasa; pahala ambapo nilikuwa nikienda kujifunza jinsi ya kutengeneza mapigo – beats – kutoka kwa mmiliki wa studio hiyo. Haikuwa ngumu sana kwa sababu tangu na tangu nilikuwa nikicheza piano nikiwa mtoto. Nilikuwa nikipiga beats wakati mmiliki anafanya shughuli nyinginezo. Hivyo ndivyo nilianza kuwa producer.

Je, ulijikuta vipi huko Zanzibar? Kwa nini?

SHIRKO (Akicheka):  Hiyo ni hadithi ndefu. Wakati nikifanya kazi katika studio hiyo, wasanii wa Mombasa walipendezwa na mtindo wangu wa kutengeneza muziki. Siku moja, mwanamuziki mashuhuri kutoka Zanzibar; ‘Berry Black’ alifika akanipata nikifanya kazi ya kupiga beats na alikuwa na nia na akaomba nimtengeneze beats kwa wimbo wake. Alirudi nyumbani na wakati wimbo ulipotokea, watu walianza kunitafuta. Nilienda Zanzibar mnamo mwaka 2004 na nikakaa huko kwa miaka mitatu kabla ya kurudi nyumbani.

Je, familia yako ilichukulia vipi maamuzi yako ya kuondoka na kuelekea visiwani Zanzibar?

Familia yangu ilinisaidia sana. Niliwashukuru, walifanya ndoto zangu ziweze kutimia kwa kuniruhusu niende.

Ilikuwaje kufanya kazi na mmoja wa wasanii wa zamani wakati huo?

SHIRKO: Ninashukuru kupitia yeye nilijifunza maana ya umoja kati ya wanamuziki. Tulifanya hata nyimbo pamoja. Ningesema alikuwa mafanikio yangu bora kama mwanamuziki na producer pia. Alikuwa msanii wa kwanza niliigiza na kutwaa tuzo ya Best Albamu katika Tuzo za Muziki za Zanzibar.

Tuambie kuhusu Yamoto Band? Ni kweli wewe ndiye mwanzilishi?

SHIRKO: Nilirudi Kenya na kukodisha studio inayoitwa Vibez Records lakini baada ya muda, tulikuwa na maafikiano na mmiliki wa mahali hapo. Nilipakia vitu vyangu tena na kurudi Zanzibar. Tayari tulikuwa tumekutana na Meneja wa studio mojawapo kule Zanzibar alipokuwa Kenya. Tulianza kuwa na ukaguzi na kutoa mafunzo kwa wasanii wa karibu ambao baadaye tutasaini. Mtu wa kwanza ambaye tulisaini alikuwa Aslay wa Yamoto Band. Wengi wao walikuwa katika kidato cha pili wakati huo. Nilianza kwa kuwarekodi kando kando na kusikiliza sauti zao. Hivyo ndivyo nilivyokuja na aina ya mtindo wa Dance Bongo Flava ambao mwanzoni ilikuwa changamoto kupata ukichezwa kwenye redio. Walikuwa bendi yenye vijana wenye umri mdogo zaidi wakati huo na walifanya maonyesho mengi katika miaka mitatu. Tena walikuwa bendi yangu ya kwanza kama ‘producer’. Walishinda tuzo mbili: Tuzo ya Kikundi Bora na Tuzo ya Wimbo Bora.

Kisha nilianza kufanya kazi na Diamond Platnumz. Nilikuwa miongoni mwa ma-producers waliofanya kazi kwenye wimbo wa ‘Kidogo’ aliowashirikisha P Square kutoka Nigeria.

Mmiliki wa Shirko Media, Awadh Salim. Picha/ Farhiya Hussein

Vipi safari yako hadi ukaanzisha studio yako huko Mombasa ‘Shirko Media’?

SHIRKO: Mama yangu alipofariki ilinibidi kurudi nyumbani na kulikuwa na pengo katika tasnia ya muziki nchini Kenya. Ilikuwa ngumu kwa wasanii wanaokua kupata nafasi, kwa hivyo niliamua kufungua studio na lengo kuu la kuwapa motisha wasanii wachanga katika safari zao za muziki.

Ni muda gani sasa tangu ufungue? Ni wasanii gani ambao umeshirikiana nao?

SHIRKO: Sasa ni miaka tatu tangu nilipofungua Shirko Media. Tunafanya kazi na wasanii wa aina za ngoma mbali mbali kutoka injili, genegetone, rap. Nimefanya kazi na Sosuun, Lady B miongoni mwa wengine. Kuhusu wasanii ninaowakuza, fahamu tu kwamba wapo wengi sana.

Je, umefanya kazi pia na wasanii wa Qasweeda? Labda sababu zako ni zipi?

SHIRKO: Kaswida – Qasweeda – ni mashairi yenye mapigo na mada za mawaidha ya Waislamu na fani hii ni mojawapo yenye wasanii wa hali ya juu lakini hawatambuliki. Ilikuwa wakati wa kuleta taswira tofauti huko nje. Sasa naweza kusema, wako pahala pazuri. Wengi wao tunawaona wakitoa burudani haswa wakati wa Eid Barazas ambazo ni jukwaa la kipekee sana. Gavana wa Mombasa Hassan Joho aliwasikia na akawapa nafasi hiyo ya kutumbuiza mbele ya umma.

Acha tuzungumze kidogo juu ya uwezo wako wa kucheza violin?

SHIRKO (Akicheka) :  Ndio, nafurahiya hiyo. Ni njia moja ninayoonyesha kama mwanamuziki.

Baada ya kufanya kazi huko Unguja na Kenya, unafikiri ‘producers’ wa Kenya wanashindwa wapi?

SHIRKO: Changamoto kuu tunayokabiliana nayo ni ukosefu wa ubunifu. Watu hawataki kuonyesha umoja na kushauriana na wengine; hali tofauti kabisa na wasanii wa Zanzibar.

Kipande chako cha mwisho cha ushauri ni kipi?

SHIRKO: Wasanii wakubwa na producers watoe fursa kwa vijana wanaokuja. Kama msanii unayeinukia, uliza maswali kila wakati, tengeneza marafiki na kuwa radhi ujifunze kitu kipya kila siku.