Makala

ANA KWA ANA: Nguli Chris Martin kaja na wazee wake wa kazi

December 6th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

STAA kutoka Jamaica Chris Martins kesho katika viwanja vya Impala Grounds mjini Nairobi atakuwa akichafua hewa kwa shoo kubwa iitwayo Big Deal Concert.

Itakuwa ni kubwa sababu mzee wa shoka aliambatana na wazee wakazi Future Fambo na D Major. Wote hawa ni wasanii wakubwa wa muziki wa reggae na dancehall hivyo kuwa na uhakika wa makamuzi ya kuumiza ubongo.

Safu hii kama ilivyo ada ya kwenda na kasi ya kukusogezea karibu matukio na mahojiano ya kina na mastaa wa sampuli hii, tulijitahidi kumfrikia Chris Martins na kupata ubuyu.

Chris hii itakuwa safari yako ya pili kutua Kenya kama sikosei?

Martins: Hapana ni mara ya tatu sasa

Katika safari zote hizo mbona hujawahi kufanya kolabo na msanii yeyote wa hapa?

Martins: Hilo ni kweli na ni aibu kubwa kwa upande wangu na nafikiri safari hii nitajitahidi nilifanyie kazi. Sio lazima msanii awe anafanya reggatone au dancehall, ilimuradi muziki ni mzuri nipo tayari kujaribu na wenyeji wangu

Unarejea Kenya baada ya miaka tisa. Katika kipindi hicho muziki wetu umebadilika sana, sasa hivi muziki wenu wa dancehall na reggae unakwenda sawa na gengetone. Hivi umepata kuusikiza muziki wa gengetone?

Martins: Aaah! Ndiyo nimefika sijatulia vizuri nikaweza kujua kipi kimenadilika toka mara ya mwisho nilipokuwa huku. Ila kama kuna aina yenu ya muziki ambayo mumeikubali nafikiri ni jambo nzuri sana na kubwa sababu hiyo itawapa utambulisho wenu. Nitapenda sana kuulewa huu muziki wa gengetone. Cha msingi tu ni uwe muziki mzuri.

Kizungu chako sio cha kawaida kutokana na lafudhi ya kwenu Jamaica. Unaweza usieleweke kwa urahisi. Umewahi kujikuta sehemu ukashindwa kuwasiliana na watu kutokana na hilo.

Martins: Nashukuru kwamba sehemu nyingi Kiingereza ndio lugha kinatumika sana na hata kama cha kwetu kina huko kuborongwa sana kutokana na mazingira tuliyokulia, angalau huwa sio vigumu mtu akashindwa kukuelewa. Yapo maneno yatampita yapo atakayoyapatia au atakisia ninachojaribu kusema na tutaishia kuelewana.

Kuna tabia hii ambapo mgeni mara nyingi hufunzwa misamiati michafu kwanza anapokuwa ugenini. Wewe umefunzwa yepi?

Martins: (Akicheka) Nafikiri hili ni tukio la kawaida na lipo kotekote hata kwetu Jamaica. Sasa mshanifunza kadhaa ila nafikiri nimesahau hehe.

Hivi uliwahi kufikiri utakuja kujipatia riziki kupitia muziki?

Martins: Kusema kweli sikuwahi kuwa na mawazo ya kuwa mwanamuziki ila nilijua napenda kuimba na najua kuimba.

Safari yangu ilianza kama ajali baada ya kushinda shindano la uimbaji kule Jamaica 2005. Lilikuwa shindano kama lile la American Idol. Sasa baada ya kushinda shindano hilo nikagundua ni jinsi gani watu walivyokuwa wakihusudu kipaji changu, sauti yangu. Upendo nilioupokea ulikuwa mkubwa mno. Ndipo sasa mawazo ya kuendelea kufanya muziki yakanishika. Sikuchagua muziki, muziki ulinichagua.

Unasema hukuchagua muziki; muziki ulikuchagua. Hii ina maana kwamba ulikuwa na dhamira ya kuwa mtu gani kabla ya muziki kukuteka?

Martins: Sijui ila pengine leo hii ningekuwa nafanya kazi benki kokote kule. Yaani kazi ambayo ningekuwa nafanya lazima ingekuwa inahusika na mahesabu. Nina digrii katika masuala ya Fulusi na niliifanya nikiwa tayari nimeanza kuimba.

Kwa hiyo ndoto yako toka mwanzo ilikuwa uje kuwa mhasibu au mtaalamu wa fulusi?

Martins: Hapana; ndoto yangu ilikuwa niwe mwanasanyasi wa kemikali (Chemical Engineering) lakini familia yangu ikawa haina uwezo wa kunilipia karo ya kozi hiyo. Hii ndiyo sababu nikaamua kushiriki hilo shindano la uimbaji nikiwa na matumaini nitashinda nipate zile hela za ushindi ili niweze kuilipia karo yangu. Lakini nafikiri baada ya kushinda mambo yakabadilika. Bado nilikwenda shuleni na kuamua kusomea masuala ya Fulusi huku nikiwa nafanya muziki.

Wazazi wako hawajawahi kuwa kikwazo katika muziki wako?

Martins: Haijawahi kutokea. Wamenilelea kanisani na hata nimeanza kuimba kanisani kabla ya kuanza kufanya muziki wa kidunia. Na hata nilipoanza kufanya muziki wa kiduni waliendelea kunisapoti wakisema kile ni kipaji ilimuradi naambia nyimbo zenye heshima.

Na kwa sababu unafanya muziki wa kidunia, je wewe ni mtu wa imani?

Martins: Tena kubwa sana naamini yupo Mungu. Naamini ndiye anayekupangia na ndiyo sababu leo tupo na wewe hapa. Kila unachokifanya naamini huwa kimepangwa na Mola tayari pasi na wewe kujua, wewe unachofanya tu kutimiza mipango hiyo.

Wapo watu wa kuchamba, kukashifu huwa hawakosagi, je kauli zao hukuathiri?

Martins: Siwezi kumkubali mtu akawa na mamlaka kama hayo juu yangu. Mawazo hasi ya mtu yeyote wala hayawezi kuniumiza sababu najiamini sana na sijaanza leo. Ndiyo maana wananiita Big Deal sababu najiamini sana.

Kweli watu wanakuchukulia kama Big Deal, wanakuchulia kuwa mfano mzuri, lakini wewe binfasi kwa wasanii wako wakubwa unaowatambua mara kwa mara unamtaja Stevie Wonder. Kwa nini?

Martins: Tangu utotoni nimeishi kusikiza muziki wake na wakati mmoja nikipiga shoo mjini Los Angeles Promota aliniambia Stevie Wonder anakuja kwenye shoo yangu. Sikuamini kwamba anaweza akawa anaupenda muziki wangu. Huyu ni Big Deal. Mmoja kati ya wasanii wakubwa kuwahi kutokea katika ulimwengu wangu wa muziki. Pia yupo Sam Cooke, Miachel Jackson kutoka Afrika Lucky Dube. Majina ni mengi ila siwezi kuwataja wote

Umetunga hiti nyingi sana ni ipi unayoweza kusema ni kubwa?

Martins: ‘Mama’ siku zote. Yule mwanamke ndiye nguvu yangu, ndio uti wangu. Nimelelewa na baba pia lakini mamangu ndiye mtu ambaye aliishi kunisukuma. Aliniambiaga nisiwahi kubali kushindwa.