Makala

ANA KWA ANA: 'Nimepiga shoo kibao ila Kenya mmenikubali'

September 13th, 2019 2 min read

Na THOMAS MATIKO

JUMAMOSI iliyopita Konshens, mkali wa Dancehall kutoka Jamaica alikinukisha katika uwanja wa Ngong Racecourse alikopiga shoo ya kufa mtu kwenye tamasha ya Hype Fest.

Ilikuwa ni safari yake ya tatu hapa nchini ila aliacha kumbukuzi usiku huo kwa aina ya utumbuizaji aliowapa mashabiki wake wengi wakiwa hawa wanaosemwa kuwa ‘Millenial’.

Konshens. Picha/ Francis Nderitu

Kama kawaida, safu hii ilikuwa kwenye maeneo ya matukio na hata kuishia kufanikiwa kupiga stori naye. Hivi ndivyo gumzo la safu hii naye lilitirika.

Natumai umefurahia likizo yako fupi Kenya?

Konshens: We acha tu! Yaani sijui nikwambieje, toka nilipotua Kenya siku tatu hizo zimekuwa za kupendeza sana. Mapokezi niliyoyapata ni ya aina yake kila nilikopelekwa. Wakenya mmenipa shavu sana hadi basi. Hakika sijutii safari hii. Nilikuwa nimeisubiria kwa hamu kubwa na kweli yamenikuta mazuri. Wakenya nyinyi watu spesheli.

Eti eeeh! Au ndio kutusanifu kaka?

Konshens: Oya naomba unisikize. Ninachosema ninakimaanisha, siwezi kuongopea niliyoyaona. Mapokezi niliyoyapata nilitegemea ila sio kwa kiwango kama cha sasa. Isitoshe, kinachowafanya kuwa spesheli machoni mwangu ni ngoma ile ya No Retreat No Surrender ambayo nilianza kuitunga nikiwa hapa nilipokuja safari ya kwanza. Ngoma hiyo ilipotoka, kule kwetu haikuvuma sana ila Kenya, ikawa bonge la ‘hit’. Hii inakuambia nini, kwamba mnanikubali sana na hiyo kwangu ni jambo spesheli sana.

Unasafiri sana duniani kwa ajili ya shoo, tupe picha ya aina ya mashabiki ambao wewe hukumbana nao?

Konshens: Acha nikwambie kitu japo utadhani ninakusanifu. Nimefikia hatua ya kuwazia kwamba Wakenya walio nje ya nchi ndio wengi zaidi kuliko mlioko huku. Sababu gani nasema hivyo? Kwa kila shoo zangu duniani, sijakosa kukutana na Wakenya. Inakuwaje mmetapakaa kihivyo? Ndio maana nikikuelezea mnanipunga sana, sitanii.

Tunashukuru. Kwa mapenzi unayosema tumekupa, unadhani wenzetu Afrika Kusini wamekosea wapi kwa kile kinachoendelea?

Konshens: Kule si ni kupumbazwa bro. Inakuwaje Waafrika tunageukiana kwa sababu za kipuzi kama zile. Tunabaguana wakati tunafanana. Haya yanatokea sababu ya kule kupumbazwa na mkoloni. Hizi ni athari zake. Wajua hata utumwa usingefanikiwa endapo Mwafrika asingemgeukia mwenzake? Haingewahi kutokea, tulihadaika. Tunahitaji kugutuka na kugundua sisi ni watu wa asili moja, asili ya mtu mweusi, haijalishi mmoja wetu anakotokea ilimuradi tu tuna ngozi sawa, tupendane.

Hebu tugeuze mita bendi kidogo na tuzungumzie muziki. Ukiwa msanii wa Dancehall uliyebobea, ni ushauri upi ambao mara nyingi wewe hutoa kwa chipukizi?

Konshens: Kama ni kuhusu muziki huwa sina la kuwaambia. Muziki hauna formula mzee. Muziki unatoka ndani ya mvunguni mwa nafsi ya mtu hivyo huwezi kujilazimishia. Huu ni kama mwito vile, wajua. Lazima kiwe ni kitu unachopenda na kukidhamiria, hiyo inatosha kukusukuma kuwa mwanamuziki mzuri.

Halafu wale madogo wa Ethic ulianzaje nao hadi kuachia ‘Figa’ Remix?

Konshens: Sikuwa nimekutana nao hadi Jumamosi (iliyopita). Ila nilitumiwa wimbo wao, nikapenda mdundo kisha nikamuuliza G Money (DJ wa Kijamaica na mtangazaji wa redio Kenya) unahusu nini sababu sikuwa naelewa yale mashairi. Baada ya hapo nilikwenda nikarekodi kipande changu nikatuma, wakaunganisha. Hawa madogo nafikiri wapo vizuri.

Ni msanii yupi mwingine Kenya ungependa kufanya naye kazi?

Konshens: Sijifungi mimi, nipo tayari kuchapa kolabo na msanii yeyote yule ilimuradi staili zetu ziingiliane na pia uhusiano wetu. Napenda kuwa mbunifu, hivyo kama yupo yeyote yule mwenye ubunifu wa aina fulani, nipo tayari kushirikiana naye.

Hivi ni lazima kila ‘video vixen’ kwenye ngoma zako awe kavalia nusu uchi?

Konshens: Hahaha! Usinichekeshe mzee. Wajua mimi ni mtumbuizaji, nipo kwa ajili ya kutoa burudani kwa kile wanachokipenda mashabiki. Isitoshe, ile ndio swagg ya Dancehall, sio video zangu tu hata za wenzangu kibao zipo vile. Wewe jaribu kuzicheki kisha utaniambia.

Wewe muuza sura sana, utakuwa ni ‘bad boy’ au ‘good boy’?

Konshens: Kwa asilimia 70, picha ninayoichora ni ya ‘bad boy’ ila isitafsiriwe ni kana kwamba sina uzuri wangu, huo upo!