Makala

ANA KWA ANA: 'Nimevunja wengi moyo kutengana na Vanessa lakini tufanyeje?'

November 29th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

KUFIKIA sasa kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa gemu ya showbiz katika Ukanda huu utakuwa unamfahamu msanii Juma Musa Mukambala au ukipenda Juma Juxx.

Wiki mbili tatu hivi, Juxx alichia albamu yake ya The Love Album ambayo imekuwa ikifanya vizuri tu.

Ni albamu yake ya kwanza tangu anajiunga na muziki. Lakini pia ni albamu anayosema inazungumzia maisha yake ya kimahusiano ikiwemo yale yaliyovunjika na kuzua gumzo sana yaliyomhusisha msanii V Money ukipenda Vanessa Mdee.

Tuligongana naye Juxx kwenye mitaa ya Nairobi akisukuma albamu yake hiyo na kuamua kutitirika naye kuelewa zaidi yaliyojiri pamoja na harakati zake za usanii:

Sielewi ni kwa nini uliamua kufanya media tour ya uzinduzi wa albamu yako huku wakati huna mashabiki wengi +254 na hata shoo hujawahi kupiga huku?

Juxx: Kila jambo huwa na mwanzo wake naamini ndio nimeanza hivi. Wajua kwa miaka hiyo imepita toka naanza gemu, nilijikita zaidi katika kujenga brandi nyumbani sasa hilo nimefanikisha na ndio nimeamua kupanua mbawa zaidi. Unaona nimefanya kolabo na Nyashinski, sasa albamu tour nimeileta huku hivyo nipe muda bro nitanyoosha.

Albamu yenyewe kubwa sana nyimbo 18, ilikuchukua muda gani kuiandaa?

Juxx: Nilianza mchakato huu miaka mitatu iliyopita. Imenichukua muda sababu nilitaka kila wimbo katika albamu ujisimamie. Wajua kuna baadhi yetu hufanya albamu na nyimbo zingine tunatunga tu ili tujalize tu lakini mimi nilitaka kila wimbo uwe na vibe yake.

Kuna wadau wanaoamini albamu haiuzi kama singo hasa kwenye soko letu hili la Afrika Mashariki?

Juxx: Sio kwa dunia tunayoishi sasa hivi, ilikuwa hivyo miaka michache iliyopita. Utandawazi haukuwa umetanda kama sasa, tekinolojia ya muziki haikuwa imetufikia kama sasa. Albamu ziliuzwa kwenye MaCDs sasa hivi zinauzwa kwenye tovuti. Mtu yeyote duniani anaweza kupakua albamu yako kiulaini sababu zipo tovuti kibao za kusambaza.

Unaweza ukajitolea mfano?

Juxx: Kabisa mwana. Nitakuambia kitu. Siku ya kwanza nilipoipakia albamu kwenye tovuti ya AudioMack zaidi ya watu milioni waliipakua chini ya muda wa saa 10 toka tuweke. Kwenye Boomplay ilipakuliwa zaidi ya mara 50,000 kwa kipindi sawia. Hizi zote ni hela mzee. Sasa hivi soko la muziki lipo kwenye utandawazi.

Nimekuwa nikichakura hapa na pale, nikagundua kuwa wapo wadau Tanzania wanaamini upo vizuri kwenye masuala ya fasheni zaidi ya muziki. Hivyo wanahoji pengine ukishika fasheni, itakuwa freshi zaidi kwako?

Juxx: (Akicheka) Hebu tuambiane ukweli tu kama sio huo muziki hao wanaoponda wangenifahamu? Kingine kwa sasa hivi huwezi ukawataja wasanii watano kutoka Tanzania wanaofanya vizuri ukakosa jina langu pale. Shoo napata kwa fujo hata wao wanalifahamu hilo. Nafikiri ishu hapa ni kwamba kiwango changu cha fasheni kipo katika levo tofauti au tu wameamua kuona sehemu moja ya maisha yangu.

Tukirudi kwenye muziki, unapenda kuimba sana mapenzi, ndiyo staili unayotaka mashabiki wakuzoee nayo au?

Juxx: Nilipoanza muziki nilijiwekea malengo. Kwanza nilitaka albamu yangu ya kwanza iwe ya mapenzi. Hata hivyo, zipo nyimbo kadhaa kama ‘Hatufanani’ ambazo sio za mapenzi.

Tukiwa hapo kwenye mapenzi, baadhi ya kazi kwenye Love Albamu ni kama vile zinamponda Vee Money?

Juxx: Sio kweli. Wajua toka naanza kufanya muziki nimekuwa kwenye mahusiano na pia ni kipindi hiki nimekuwa nikirekodi nyimbo hizi. Nyingi unakuta zimejengekea kulingana na mambo niliyokuwa nikipitia kimahusiano kwa wakati huo.

Toka umeachana na Vee Money unaonekana mbaya sana mashabiki wengi wanakuchamba wewe?

Juxx: Najua tulikuwa kapo ya nguvu na wengi tuliwavunja moyo baada ya kutengena lakini ilishatokea tufanyeje sasa?

Wanaokuchamba wanaamini ulikuwa mbaya sababu ni kwa nini uliingia kwenye mahusiano mapya haraka?

Juxx: Wajua watu wengi wananichukulia mbaya ila hawajui chanzo cha sisi kutengana na Vee Money. Baada ya kutengena tuliagana tukae kimya lakini miezi michache akaamua kutoboa siri sasa na mimi ndipo nikaamua kumweka mpenzi wangu hadharani na watu wakaanza kuniona mbaya.

Sijakuelewa, Vee Money ndiyo sababu yenu kuachana?

Juxx: Ndio, mwenyewe aliniketisha kwenye kikao akaniambia anataka tuuvunje uhusiano sababu mambo yake mengi yalikuwa yanakwama.

Pili aliniambia pasta wake kamwambia kapungukiwa katika imani sababu kajichanganya kwa kuishi na mwanamume kwa miaka mitano bila ndoa. Iliniuma lakini sikutaka iwe ni mimi nimemfungia riziki sasa kama anasema kuwa na mimi inakwamiza vitu vyake nikaona freshi. Nakumbuka nikimuuliza kabisa ikiwa anahitaji tutengane kwa muda. Alichonijibu ni kwamba anataka tuachane kabisa. Ingekuwa wewe ungefanyaje?

Unahisi vipi kumwona akiwa na Rotimi?

Juxx: Ninachoweza kusema ni hiki, shemeji yetu amtunze mtoto wetu vizuri sababu Vanessa ni binti mzuri. Asingekuwa mzuri singekuwa naye miaka yote hiyo. Bahati mbaya hatungeweza kuendelea ila kila la kheri kwao.