Makala

ANA KWA ANA: Resipe anazotengeneza ni mwongozo wa kipekee kwa wapishi

September 27th, 2020 2 min read

Na WANGU KANURI

MAPISHI bora humvutia kila mtu anayejua umuhimu wa lishe kuanzia jinsi chakula kinavyopikwa hadi vile chakula kinavyoandaliwa.

Isitoshe, vyakula vingi huwa na resipe ambayo mpishi anaweza kutumia kama mwongozo ili kupata ladha mahususi aliyokusudia.

Wanaozitengeneza resipe hizi huwa na matumaini ya kuwasaidia watu wengi ili wao wafahamu jinsi ya kupika chakula chochote kwa njia mbalimbali.

Upishi ni sanaa ambayo huhitaji ubunifu na kujaribu kwingi bila ya kukata tamaa.

Taifa Jumapili inamwangazia mmoja wa waundaji wa resipe ambaye uzoefu wake katika upishi umemsaidia kutengeneza resipe zake.

Tueleze kwa kifupi, wewe ni nani?

PRISCILLA ARIOKOT: Jina langu ni Priscilla Ariokot na mimi ni mzawa wa Uganda lakini nilihamia Kenya mwaka wa 2014. Mimi ni mwalimu, mtayarishaji wa resipe na napenda kuandika kuhusu vyakula mbalimbali katika blogu yangu. Resipe zangu zinaweza kupatikana katika kurasa zangu za Instagram na Facebook ambazo ni plate_up na Priscilla Ariokot mtawalia.

Mbona ukajitosa katika upishi na lishe?

PRISCILLA ARIOKOT: Ninapenda kupika na nina ari ambayo ilisisimuliwa kwa kutazama vipindi vya mapishi katika runinga na katika hoteli ambazo nilizuru nyumbani kwetu, Uganda.

Umeweza kuunda resipe yako binafsi?

PRISCILLA ARIOKOT: Ndio. Nimeweza kuunda resipe zangu ambazo kwa sasa siwezi kuhesabu.

Ni resipe gani inayokusisimua mno?

PRISCILLA ARIOKOT: Resipe ambayo ninapenda sana ni ile ambayo nitatumia kuku; iwe kuandaa supu ya kuku ama kuchoma kuku au kitoweo cha kuku. Kwa sasa resipe ninayoipenda zaidi ni kupika kuku kwa kutumia nanasi.

Wapishi wengi waliosomea upishi huwa na viungo ambavyo hutumia kila wakati wakiandaa chakula chao. Je, ni viungo gani haviwezi kukosa katika chakula chako?

PRISCILLA ARIOKOT: Kila chakula ninachokipika sharti kiwe na mchanganyiko wa kitunguu saumu na tangawizi, jira na bizari aina ya simba mbili.

Chakula kilivyoandaliwa kinaweza kukutia hamu ama kukukosesha ile hamu. Je unaafikiana na kauli hii?

PRISCILLA ARIOKOT: Ndio, ninaafikiana na kauli hii na kwa hivyo mimi huhakikisha kuwa viungo vyote nitakavyotumia kwa mapishi yangu ni safi. Isitoshe, mimi huandaa chakula changu vizuri kwani mtu hula kwanza kwa macho kabla ya kuanza kula chakula chenyewe.

Chakula. Picha/ Hisani

Ni chakula gani ambacho kilichochea hamu yako ya kutaka kupika?

PRISCILLA ARIOKOT: Chakula kilichochochea hamu yangu ya kutaka kupika ni supu ya mchanganyiko wa karoti, viazi, maharagwe na vitunguu ambacho resipe yake ilikuwa katika kipindi kimoja televisheni. Nilipojaribu kupikia babangu supu hiyo kama ilivyoonyeshwa televisheni, ladha yake haikuwiana lakini akanipa moyo. Kwa kuwa kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa kupika, nikaanza kurekebisha kosa zangu za jikoni. Isitoshe, nikajitosa katika kujua kupika na kujifunza njia mbadala za kupika chakula mbalimbali.

Katika uundaji wa resipe, je ni changamoto gani unazopitia?

PRISCILLA ARIOKOT: Ninapokuwa nikiunda resipe changamoto ninazokabiliana nazo ni kama kusawazisha viungo vya poda na pia kujaribu viungo ambavyo sijawahi jaribu kupikia.

Ni chakula gani ambacho umewahi kula na hukupenda ladha yake na hata ukijaribu kupika mwenyewe bado hakuna ladha?

PRISCILLA ARIOKOT: Sipendi maini. Nimejaribu hata kujipikia mwenyewe lakini sijawahi kupenda ladha yake.

Ni kosa gani ambalo umewahi kulifanya jikoni wakati ukiandaa chakula?

PRISCILLA ARIOKOT: Nilikuwa nikipika tambi (spaghetti) kitambo kidogo; nikachemsha maji na kuzitumbukiza mle kisha nikasahau. Niliporejea, nilipata zimekuwa kama uji. Niliziepua na kuwapa kuku waliokuwa wamefugwa pale nyumbani.