Makala

ANA KWA ANA: 'Si mgonjwa wala sikumbaka yeyote'

June 28th, 2019 3 min read

Na THOMAS MATIKO

IKIWA ni zaidi ya miezi mitano sasa tangu itokee ile skendo ya ngono iliyomuhusisha msanii wa injili DK Kwenye Beat alikoshtumiwa kumwambukiza binti mmoja kutoka Nakuru ugonjwa hatari wa zinaa ‘Herpes’, mwanamuziki huyo kafunguka jinsi maisha yalivyombadilikia toka kashfa hiyo imkute.

Vipi, ni kama vile zoezi umesusia sababu mwonekano wako kama vile upo pale pale?

DK: Unaifanya ikae vibaya ni kama vile mimi ni mnene sana. Zoezi bado nipo sema chakula pia ni kitamu na sijawahi kosa hamu.

Halafu hicho kimya nacho, umepotea sana?

DK: Kweli nimepotea kwa muda wa miezi sita ila nipo nashukuru.

Ulikashifiwa sana, mtandao haukutulia toka ile skendo hasa ikizingatiwa wewe ni msanii wa injili?

DK: Kweli mtandao ulikuwa stima. Wajua katika maisha yangu yote sijawahi kuwa na skendo, hii ilikuwa ya kwanza na nzito sana.

Naomba utuweke sawa, kilichotokea ni kipi?

DK: Una muda wa kutosha kweli sababu ni stori ndefu sana. Ila acha nijaribu kuifupisha. Ilikuwa wiki ya mwisho ya Januari ilipotokea ghafla nashtumiwa kubaka na kumwambukiza msichana fulani ugonjwa wa zinaa. Ishu ililipuka kwenye blogu moja. Ilipotoka, ikawa kubwa sana na mimi nikihusishwa. Kile nilichofanya baada ya kutrendi ni kuomba msamaha. Kile kitu ambacho watu hawakuelewa ni kwamba mimi kuomba msamaha hakumaanishi nilikuwa nimekosea. Nilichokifanya ilikuwa ni jitihada za kujaribu kulinda heshima yangu. Isitoshe, lilikuwa ni suala nyeti lazima ningezungumza.

Lakini pia ilivuja audio fulani baada ya skendo uliposikika ukijitapa kwamba yule binti hawezi kukushtaki sababu hana ushahidi kuwa ulimshinikiza kufanya naye ngono. Na pia ulisikika ukijigamba kwamba kweli ilitokea?

DK: Haikuwa mimi, haikuwa sauti yangu, nami niliumwa pia. Wajua katika ulimwengu wa sasa tunamoishi yeyote anaweza kuwa hata Raila. Haikuwa mimi kabisa na ndio sababu wakati naomba msamaha sikuigusia audio hiyo kwa kuwa sikuhusika.

Huyu binti mlifahamianaje?

DK: Nilimfahamu kupitia mtandaoni hata zile chati zilizowekwa kunianika hazikuwa za simu zilikuwa za DM ambapo yeyote anaweza kuwasiliana naye na kwa kawaida maongezi yenu yatakuwa ya kawaida sana. Ila stori ilipotoka ikawa ni tofauti, kwamba alikuja mara ya kwanza kumcheki Hopekid na aliporudi safari ya pili ndipo nikambaka. Miezi mitatu baadaye akasema nimemwambukiza ‘herpes’ kisha baada ya miezi miwili zaidi ndipo stori nzima ikatoka.

Ila wajua lisemwalo lipo?

DK: Kweli ila acha niweke hili wazi. La kwanza, sikumbaka mtu yeyote, la pili sikuwa mgonjwa na nina vipimo hapa na nipo tayari kuviweka wazi. Na kama kuna anayeshuku, basi nipelekwe kortini niamrishwe kupima tena sababu nimeambiwa ni kirusi na kikiingia mwilini hakitoki milele.

Na la tatu huyu binti sio mpenzi wangu na wala sikushiriki naye ngono ila namjua. Huyu binti alitumiwa bila kujua kutuchafulia jina mimi na Hopekid.

Alitumiwa na nani?

DK: Waliohusika ni baadhi ya wasanii wa injili tena maarufu ambao sina nia ya kuwataja kutokana na imani yangu ya Kikristo.

Skendo hii imekuathiri kivipi?

DK: Nimepoteza heshima yangu, nimepoteza dili kibao, pia watu niliodhania ni marafiki walinikimbia. Hata baadhi ya redio na TV zimefungia kazi zetu kuchezwa. Hatujakuwa tukipata shoo, kwa kweli kimekuwa kipindi kigumu kwetu. Kwa mwezi mzima nilishindwa kutoka nyumbani. Ilikuwa moto.

Umejifunza nini kutokana na kashfa hii?

DK: Kwamba sina marafiki. Hata wasanii wenzangu wa injili wengi walinitenga kwa kuhofia nao isiwageukie. Wale wachache waliosimama na mimi ni Size 8 na mume wake DJ Mo, Bahati (Kevin), Ringtone na Guardian Angel. Zaidi yao, ni familia yangu.

Mpenzi wako Shanice je?

DK: Bado yupo tena kwa sana.

Hii skendo ilimwathiri vipi?

DK: Ilimuumiza sababu ana hisia, ana familia na anao marafiki. Ishu kubwa hata sio yeye, wapo wale marafiki watakaotia sindano sana, wapo baadhi ya wanafamilia ambao hawataelewa na zote hizi zilikuwa sehemu ya changamoto tulizopita pamoja.

Mumekuwa pamoja kwa muda gani?

DK: Miaka saba sasa toka tumekutana nikiwa sina hela wala jina.

Muda wote huo mbona msioane?

DK: Ninachojua ni kwamba tutafanya harusi Desemba ila mwaka ndiyo sijui. Lakini pamoja na yote Mungu atatusaidia na kama tumeupita huu mlima tuliokuwa nao juzi, basi harusi ipo.

Baada ya yote haya unafanya nini kusafisha jina lako?

DK: Hilo haliwezi kubadilika machoni pa wengi ila kwa yote nimeamua kumtumainia Mungu sababu anajua ukweli upo wapi.