Makala

ANA KWA ANA: Wawakilishi wa +254 'Amazing Voices' huko Sauzi wazungumza

March 13th, 2020 2 min read

Na THOMAS MATIKO

KUNA shindano linaloendelea la uimbaji Old Mutual Amazing Voices ambalo linakaribia kufika fainali.

Shindano lenyewe linafanyika kule Afrika Kusini na linahusisha mataifa manne Ghana, Zimbabwe, Afrika Kusini na Kenya.

Shindano hili lilianza mwaka jana ambapo makundi ya wasanii chipukizi yaliteuliwa na kuanza mashindano ya michujo na mpaka sasa yamesalia makundi 12 yaliyoingia fainalini.

Kwenye makundi hayo 12, lipo moja la Kenya Wanavokali waliofanikiwa kufika fainalini baada ya wenzao Solid Rock Band na Duaro Harmonies kutupwa nje.

Mshindi wa shindano hilo ataondoka na kitita kizito cha Sh10 milioni. Safu hii iliketi na madogo hao chipukizi na kupiga nao stori:

Hivi mlijipataje kwenye shindano hili?

Wanavokali: Ilipotangazwa tukasikia, tukaamua kwenda kufanya usahili, yale majaribio na majaji Wakenya wakiongoza na Kavutha pamoja na msanii Sanaipei Tande wakaridhishwa na kiwango chetu. Tukabahatika kujiunga na wenzetu Solid Rock Band na Duara Harmonies kutoka Mombasa.

Hadi kufikia sasa shindano limewapelekaje?

Wanavokali: Mwanzo kabisa imekuwa ni fursa ya kipekee kwetu sisi kutufungua mawazo katika ulimwengu wa muziki hasa ukizingatia kuwa sisi ni wasanii wapya kabisa.

Tumekuwa pamoja kwa muda usiozidi mwaka hivyo tumeweza kujifunza mengi. Pia tumepata fursa ya kusafiri, kutangamana na tamaduni za wenzetu tunaoshindana nao kutoka mataifa mengine ya Afrika. Kikweli Bara hili lina vipaji. Lakini pia tumepata mafunzo ya hali ya juu kutoka kwa wakongwe wa tasnia ya muziki kama vile Zwai Bala ambaye ndiye Mkurungezi wa shindano. Matumaini yetu ni kwamba tutashinda na tuweze kuleta hela hizo nyumbani.

Washindani 12 fainali, hivi mna imani mtashinda?

Wanavokali: Tunajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri katika shindano, hilo naweza nikawahakikishia. Shindano linaelendelea na mashabiki wanaweza kutufuatilia kwenye Maisha Magic East Channel waone tunachokifanya.

Ikitokea mshinde, hela hizi Sh10 milioni mtafanyia nini?

Wanavokali: Hela hizo kwa kweli zitasaidia sana kuanzisha taaluma yetu ya muziki kama kundi. Lengo letu ni kuiteka sio tu tasnia ya Kenya bali Bara Afrika. Tunajiamini sana katika kile tunachokifanya. Kwa uwezeshaji huo, tutaweza kujipanga vizuri katika kujijenga kiusanii, kikazi kusukuma muziki wetu.

Lengo la kila mshiriki ni kushinda, ikitokea vinginevyo, mna mipango gani?

Wanavokali: Tunaamini tayari tumeshinda. Kufika umbali huu tuliofika kwa sasa ni ushindi tayari. Ushindi wa shindano itakuwa ni bonasi kwetu. Kikubwa zaidi hatutaondoka bure sababu tayari tumepokea mafunzo na ufundi wa hali ya juu kutokana na shindano. Pia tusisahau kwamba shindano hili ndilo limetupa fursa ya kujitambulisha kwenye gemu.

Kuna mikosi ya makundi kusambaratika hapa nchini, Wanavokali mnahisi mtadumu?

Wanavokali: Tunaamini tutadumu. Tupo tofauti kabisa. Huu tu ni mwanzo wetu. Tumekuwa pamoja kwa miezi sita na katika muda huo tukapata fursa ya kuteuliwa katika shindano hili. Hii ina kuonyesha kuwa tupo vizuri na kwa kuwa lengo na nia ya kila mmoja wetu ni kuzidi kusukumana, sioni tukisambaratika.

Makundi mengi yaliyotangulia yaliwahi kutoa kauli kama hizo zenu, ni nini haswa kinachowafanya kuamini mtadumu?

Wanavokali: Kwa kweli masuala ya makundi ni magumu sana. Ila tunaweza kusema ni kama mahusiano ya kimapenzi. Kuna kipindi mpo vizuri wakati mwingine mnakorofishana. La muhimu hapa ni kujua ni namna gani mnatatua matatizo yenu pale mnapopitana. Mpaka sasa tumejitahidi kujielewa kama kundi mapungufu yetu na kuyafanyia kazi. Hivyo tunaamini kuwa tutaweza kudumu.

Hivi mna uhakika ya kutoboa kwenye tasnia ya muziki wa Kenya?

Wanavokali: Kabla hatujaunda kundi, kila mmoja wetu tayari alikuwa ameanza kufanya muziki. Kuna baadhi yetu walikuwa wasanii wa kujitegemea, kuna wengine walikuwa ni wasanii wa bendi za wasanii wakubwa kama Nyashinski, Nameless, Akothee, King Kaka, Mercy Masika, Esther Wahome miongoni mwa wengine. Hivyo tuna ufahamu wa ni nini cha kutegemea kwenye gemu ya Kenya. Tupo tayari.