Makala

Anafuata ndoto zake licha ya kutengwa na mama yake tangu akiwa mtoto

November 12th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

Baada ya kuwa chuoni kwa kipindi cha muda wa miaka minne mfululizo Faith Jeruto ana kila sababu ya kutabasamu.

Mwisho mwa juma lililopita, Jeruto ambaye amekuwa akisomea Shahada ya Masuala ya Uchoraji wa ramani ya barabara na nyumba katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT), alifanya mtihani wake wa mwisho kuhitimu kozi.

Kwa sasa anasubiri matokeo ya mtihani na hafla ya mahafali kufuzu ili kupokezwa cheti. Imekuwa safari ya milima na mabonde, kwa mwanadada huyu mwenye umri wa miaka 26.

Akiwa mwanambee, yaani kifungua mimba katika familia ya watoto sita, anasema kusoma masomo ya msingi na ya upili, ilikuwa kwa neema za Mwenyezi Mungu.

Ari ya kuafikia ndoto zake maishani hata hivyo iliendelea kumtia motisha kubukua vitabu, licha ya mahangaiko.

Mamake ni mwalimu wa shule ya msingi na ambaye ameajiriwa na tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC), ila anasema licha ya kuwa mwanawe mzawa, hajapata mapenzi ya mama kutoka kwake, kwa kile anataja kama “sielewi kwa nini anichukie bila sababu”.

Anafichua kwamba, watoto wanne wa kwanza, Faith akiwemo ni wa baba tofauti. Hata hivyo, hilo kwake si hoja “kwani ni mama mzazi na ninamheshimu na nitaendelea kumheshimu”.

Wawili wa mwisho ni wa baba mmoja, na ambaye anasema ni Mzee mwenye busara ambaye amejinyima mengi ili kuona kuwa anaafikia ndoto zake za kuwa saveya.

Kulingana na Faith, baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, alipata ujauzito kufuatia uhusiano wake na barobaro anayemtaja alishinda na kumiliki moyo wake.

“Urafiki wetu ni wa tangu zamani tukiwa wadogo kiumri. Awali sikumpenda, lakini muda ulivyozidi kusonga mapenzi yake moyoni mwangu yalikua na ndivyo nilijipata kumuamini hatimaye nikaishia kuwa mama ya mvulana wake,” anaelezea.

Ni hatua ambayo nusra itishie kuzima ndoto zake, akikumbuka masaibu aliyopitia mikononi mwa ninake. “Nyakati zingine nilikuwa nafikiria kutoa ujauzito huo, japo kwa sababu mimi ni mcha Mungu, nikatupilia mbali wazo hilo,” anasimulia, akionekana kulijutia, laiti angalijua aliyebeba ni malaika.

Mvulana wake ambaye kwa sasa yuko chekechea, ni staa mcheshi, mwerevu, na anayemtia tabasamu anapokumbuka masaibu aliyopitia, jaribio la kubakwa na mmoja wa ‘baba zake’ likitonesha makovu ya kidonda cha mahangaiko akiwa kikembe.

Ni maovu anayosema aliyafichua akiwa na umri wa miaka 19, ila hakuambia mamake. Licha ya dhuluma na unyama huo, Faith anasema alimsamehe ‘babake’ huyo.

Alipojiung na JKUAT, haikuwa rahisi. “Mama aliweka wazi kuwa hatanisomesha tena, nichague kuoleka,” anadokeza.

Mwanadada huyu ambaye ni mkwasi wa ujasiri na mkakamavu, anasema alipata ufadhili kupitia wasamaria wema, michango na baadhi ya wanafamilia, na kila anapopiga Dua kwa Mola anamuomba kumbariki na kumpa maisha marefu nyanyake, mzawa wa mama, ambaye amesimama kidete naye.

“Mtihani wa mwisho chuoni, nyanya aliuza ng’ombe wake ili niruhusiwe kuufanya. Mungu akinijaalia nipate ajira, atakuwa miongoni mwa nitakaorejeshea mkono na kumpiga jeki,” anasema.

Faith anaiambia Taifa Leo kwamba amekuwa akitegemea vibarua vya hapa na pale kujiendeleza kimaisha, kukithi mwanawe riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Aidha, anadokeza kwamba hufulia watu nguo (dobi), kushiriki vibarua vya ujenzi na nyakati zingine kupata vibarua vya kuchora ramani ya barabara na majengo.

Huku akisubiri kufuzu taaluma aliyosomea, Faith anasema muhimu kwa sasa ni kutafuta jukwaa kujiimarisha kimaisha aweze kujisimamia.

Anasema hachagui kazi muradi iwe ni halali na inayoridhisha Mwenyezi Mungu. “Sichagui ajira, iwe ya dobi, mijengo, kwenye hoteli…bora nipate riziki na kujiendeleza kimaisha pamoja na mtoto wangu,” aelezea.

Huku akionekana mwenye maono chungu nzima, matamanio yake yakiwa kuanzisha taasisi itakayonusuru watoto waliotengwa na jamaa zao, Elizabeth Mwangi, muuguzi mstaafu, mshauri wa masuala ya ndoa na pia Mwanasaikolojia, anahimiza msichana huyu kupata ushauri nasaha.

Bi Elizabeth anasisitiza haja ya kufarijiwa na kuhimizwa kufungua chapta nyingine ya maisha. “Ukweli ni kwamba kusahau matukio ya hujuma na dhuluma kama vile kubakwa na kupitia vita vya kijinsia katika ndoa si rahisi kusahau. Waathiriwa wanapaswa kukumbatiwa na kupata ushauri nasaha kuwasaidia kusahau waliyopitia,” mtaalamu huyo anasema.

Faith Jeruto anasema kilichomuwezesha kufikia aliko kwa sasa, ni imani kuu aliyo nayo kwa Mungu. “Kila ninapoamka alfajiri na mapema na kabla ya kulala, lazima nisali. Hakika ni kwa neema zake nimeweza kufika niliko,” anasema.

Anasema ni kwa muda tu awe miongoni mwa wanawake nguzo kuu nchini.