Michezo

Analenga kuinua mchezo wake kufikia Marcus Rasford

November 11th, 2020 2 min read

Na PATRICK KILAVUKA

Mwanasoka chipukizi Andrew Mulwa, 8, mwanafunzi wa Gredi ya Pili, Shule ya Msingi ya St Joseph ACK, Kabete na timu ya Royal Soccer Academy ambayo inafanyia maozezi uwanja wa AHITI, Kabete alijua fika kwamba amejaliwa kipawa cha kandanda. Japo aliamini safari ya kila kitu huanza na hatua moja na ameona dau lake likitimia.

Mbali na kuwa na matumaini kwamba, siku zijazo taaluma ya soka itakuwa pua na mdomo kwake kwa sababu kuna wachezaji walioanza mashinani na wakainuka kuwa wachezaji wanaotetea uzalendo nchini na kucheza hata ughaibuni. Miongoni mwao; Michael Olunga, Victor Wanyama Mugubi, Dennis Oliechi na Ayubi Timbe.

Alianza kuwa na kiu ya kujua kabumbu akiwa na miaka miwili. Hata hivyo, alijawa mori ya kucheza akiwa na miaka mitano hivi. Anasema alikuwa anaenda uwanjani kuona jinsi soka inavyosakatiwa.

Kwa kweli kiu na nia ya kucheza mpira ilimsukuma kocha Boniventure Maruti kutambua ukweli wa mambo kwani, kila mara mpira ulikuwa unaenda nje ya uwanja, alikuwa anauchukua na kuwagongea wachezaji uwanjani.

Ishara ya kwamba matamanio ya kugusa boli yalikuwa ya juu na Hali hii ilimzuzua kocha huyo sana kumpa jukwaa la kujigundua zaidi na akaimarisha mahusiano naye na kuanzisha mikakati ya kumkuza kivipaji.

“Mchezaji huyo ni wa kushangaza kwani alitambua kwamba kuwa uwanjani na wachezaji walio timuni Royal Soccer Academy kungewezesha kumpa maarifa ya kujenga uwezo wake wa kustahamili changamoto za kandanda, ” asema kocha Maruti ambaye amemchonga Mulwa hadi kufikia kiwango cha kuwa mshambulizi hodari.

Straika Andrew Mulwa akiwa wa nne kushoto pichani kikosini. Picha/Patrick Kilavuka

Isitoshe, amenogwa na mawaidha jinsi ya gawa pasi za hakiki, kupiga makombora, kuimarisha chenga mufti na kujua namna ya kujisimamisha vizuri kama straika uwanjani na kuzua msisimuko.

Hujifua sana katika mazoezi kila jumatatu hadi Ijumaa wakati huu ambapo wamo katika likizo ndefu na tayari ufumaji wake unashuhudiwa viwanjani kwani, ametia kimiani magoli sita ya kiustadi katika michuano ya kujipma nguvu.

Anasifiwa na timu meneja Vincent Ayumba kutokana weledi wa kipaji chake hususa afumapo tuta kwa ufundi usiomithilishwa.

“Tulimchagua nahodha wa timu kwa sababu anajukumika sana na ana uhusiano mzuri. Isitioshe, ni msikivu wa mawaidha na mashauri hali ambayo imerahisisha jukumu lake kikosini,” anakariri mdau Ayumba.

Licha ya umri wake, mwanadimba huyu hujumuishwa katika kikosi cha wasiozidi miaka kumi na mitatu na hufanya maajabu katika timu hiyo kutokana na miguso yake na ulengaji wa shabaha.

Anasema kucheza na timu ya waliokomaa, kunampa maarifa zaidi, kujenga usuli na kujifunza kukabili changamoto hali inayompelekea kufungua mwanya wa kufikia mchezaji kama mtingaji Marcus Rashford wa Uingereza kutokana na mifumo yake ambayo anapachikia hata Machester United mabao.

Mbali na mchezaji huyo, ana matamanio ya kuchezea FC Talent chini ya ukufunzi wa Patrick Kegode na hata kuvuka daraja kuchezea kikosi cha kitaifa Harambee Stars au kwa majaliwa ya Mola kuyoyomea ughaibuni kustawisha mizizi ya soka na kuchora Kenya kwenye ramani ya kimataifa.

Kutizama boli ya kimataifa anasema kumekuwa upenyo wa kutafakari zaidi katika angaa ya ulimwengu wa kabumbu.

Kama hafanyi mazoezi, wala kusoma au kucheza mechi ya kirafiki, mwanasoka huyu hupenda uraibu wa kutizama kipindi cha watoto Akili Akili