BENSON MATHEKA Na CECIL ODONGO
KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga anategemea washirika waliobaki katika maeneo tofauti ya nchi kufanikisha uasi wake dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.
Washirika hao ni mseto wa vigogo wa kisiasa wa vyama tanzu vya muungano wa Azimio na wabunge chipukizi.
Baada ya baadhi ya wandani wake katika maeneo mbalimbali kuhamia mrengo wa Kenya Kwanza, Bw Odinga amewakumbatia wanasiasa ambao wanaonekana kurithi nafasi za waliomhepa akilenga kudumisha umaarufu wake wa kisiasa.
Katika eneo la Magharibi, waziri huyo mkuu wa zamani anamtegemea aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa na aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya. Kupitia wawili hao, Bw Odinga analenga kudhibiti ushawishi wake wa kisiasa katika eneo ambalo limemuunga mkono tangu 2007.
Bw Odinga jana Ijumaa aliandamana na wawili hao katika mkutano wa kisiasa kaunti ya Migori ambapo walisisitiza kuwa wataungana naye katika uasi dhidi ya serikali.
Bw Odinga alitangaza kwamba, miongoni mwa uasi utakuwa ni kususia bidhaa za kampuni “ zinazotumiwa vibaya na Kenya Kwanza”.
“Hivi karibuni makao makuu yetu yatatangaza bidhaa za kampuni ambazo wafuasi wetu watasusia,” akasema.
Katika eneo la Ukambani, Bw Odinga anategemea Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na Seneta wa Kitui Enock Wambua na mwenzake wa Makueni Dan Maanzo.
Baada ya Rais Ruto kunyakua wabunge wa chama cha Jubilee Katibu Mkuu wake Jeremiah Kioni na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua wamebaki katika Azimio huku kukiwa na kila ishara kwamba, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anaunga uasi huo.Katika mkutano wa jana, Bw Kioni aliwasilisha salamu za Bw Kenyatta huku akisema eneo la Mlima Kenya linaunga uasi unaoongozwa na Bw Odinga.
Katika ngome ya Rais Ruto ya Rift Valley, Bw Odinga anaungwa mkono na Seneta wa Narok Ledama Ole Kina ambaye jana aliwataka Wakenya kujitokeza kuunga Raila ili kuokoa nchi yao izizamishwe na “utawala mbaya”.
Baada ya aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuonekana kutojihusisha na siasa za Azimio la Umoja, Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo, Mbunge Badi Twalib na Seneta Mohamed Faki wamebaki kuwa washirika wa kiongozi wa chama chao Ukanda wa Pwani.
Katika kaunti ya Nairob Bw Odinga anategemea wanasiasa vijana kama Seneta Edwin Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na mwenzake wa Makadara George Aladwa.
Bw Odinga bado ana ushawishi mkubwa wa kisiasa Nyanza licha ya baadhi ya viongozi kuelekea upande wa serikali. Ili kudumisha ngome yake, anawalea viongozi vijan kama kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi na Seneta Moses Kajwang’ wa Homa Bay.
Kwa mujibu wa Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Martin Andati, Bw Odinga anahitaji wanasiasa hao kuleta dhana kuwa bado umaarufu wake haujatikiswa hata baada ya wengine kuunga serikali.
Hata hivyo, Bw Andati anasema hoja kuu ni kuwa hata bila viongozi hao, waziri huyo mkuu wa zamani anawategemea wananchi kusukuma ajenda yake dhidi ya utawala wa Rais Ruto na anaekelea kufaulu kufanya hivyo.
“Ukitathmini siasa za Raila kwa miaka hii yote, utagundua kwamba huwa anahakikisha ana wananchi mwanzo kabla ya viongozi. Hii ndiyo maana hata baada ya baadhi ya wanasiasa kuhama bado anaungwa mkono wa raia kutoka maeneo hayo na hilo linadhihirika kutokana na idadi ya wanaojitokeza katika mikutano yake,” akasema Bw Andati.
Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Mark Bichachi naye anasema kundi la viongozi chipukizi ambao Raila amekumbatia, hawana umaarufu wao kivyao hata katika maeneo yao.
“Ukiangalia Eugene, hana umaarufu wowote Magharibi ila jina lake lina uzito tu kitaifa. Katika mapambano dhidi ya serikali ni uzito na ufuasi wa kitaifa ambao umesaidia Raila miaka yote na hilo litamsaidia hata wakati huu,” akasema Bw Bichachi.