Habari Mseto

Anasisitiza atajua nampenda akionja asali

January 2nd, 2024 1 min read

Kwako shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Ajabu ni kwamba bado hajaamini kuwa nampenda ilhali nimekuwa nikimhakikishia kila tukiwa pamoja. Anasisitiza atajua nampenda akionja asali. Hiyo ni kweli?

Usikubali kuchezewa akili na mwanamume huyo. Kitendo hicho hakiwezi kutumiwa kuthibitisha mapenzi ya mtu kwa mwenzake. Wengi hushiriki kama biashara. Kama haamini unampenda, achana naye.

Nataka ‘tuchill’ hadi tuoane, lakini haniamini!

Shikamoo shangazi. Nina miaka 25 na nina mpenzi. Ndiye wangu wa kwanza na nimemwambia hatutawahi kushiriki mapenzi hadi atakaponioa. Lakini haniamini. Nifanye nini?

Sijui mpenzi wako ameona ama kusikia nini kukuhusu hivi kwamba haamini unavyomwambia. Kama hana sababu ya kukushuku, basi anasumbuliwa na wivu tu. Shikilia msimamo wako, hatimaye atakubali.

Sijafanikiwa kupata mke

Kwako shangazi. Nimetafuta mke kwa miaka mitatu sasa na sijafaulu. Nimependana na wanawake kadhaa lakini wananiacha baada ya muda mfupi tu. Nina wasiwasi, nishauri.

Ni jambo la kawaida kuwa na wapenzi kadhaa kabla ya kupata mwenzako wa maisha. Anayetafuta hachoki. Miaka mitatu ni muda mfupi sana. Usikate tamaa, hatimaye utapata.

Kelele zake chumbani zinaniaibisha kiasi

Hujambo shangazi? Mpenzi wangu hunitembelea karibu kila wikendi. Kila akija majirani huwa hawalali kwa sababu ya kelele zake chumbani. Hakuna anayelalamika lakini naona aibu. Nifanyeje?

Itakuwa vyema uzungumze na mpenzi wako ajue unavyohisi. Labda anaweza kujizuia. Na iwapo hawezi na hutaki kuendelea kusumbua majirani, chumba hotelini kinafaa kwa shughuli hiyo.