Anaswa akimfanyia babake KCSE

Anaswa akimfanyia babake KCSE

NA WAANDISHI WETU

WATAHINIWA 831,015 leo Jumatatu wameanza rasmi mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) kote nchini, huku serikali ikiahidi kuweka juhudi kali kuzuia visa vya wizi wa mitihani.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, amekuwa katika Kaunti ya Mombasa, ambapo amewaongoza maafisa wakuu katika wizara hiyo kusimamia uendeshaji wa mtihani huo katika sehemu tofauti nchini.

Hata hivyo, mwanamume, 26, amekamatwa na polisi katika Kaunti ya Busia, baada ya kunaswa akiufanya mtihani huo kwa niaba ya babake.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Matayos, Kipchumba Ruto, amesema kuwa mshukiwa, aliyetambuliwa kama George Barasa, na aliyekuwa mwanafunzi wa zamani katika shule ya upili ya Bujwang’a, alitumia barua ya kusubiri kupata kitambulisho kuingia katika kituo cha kufanyia mtihani.

Babake mshukiwa, Josephat Basoga, 44, amejisajili kama mtahiniwa wa kibinafsi katika shule ya Upili ya Our Lady of Mercy, mjini Busia.

Katika Kaunti ya Meru, Naibu Waziri wa Elimu, Dkt Sarah Ruto aliongoza usambazaji wa karatasi za mtihani huo katika Kaunti Ndogo ya Meru ya Kati.

Dkt Ruto amesema wamejitolea kuhakikisha mtinani huo unaendeshwa katika mazingira salama, kwani ni visa vichache tu vya udanganyifu vilivyobainika wakati wa Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE).

“Tunataka kuhakikisha kuwa kila mtahiniwa anafanya mtihani huu bila kujali ikiwa ni wajawazito au wako hospitalini,” akasema Dkt Ruto.

Dkt Ruto amesema kuwa licha ya changamoto zilizosababishwa na janga la virusi vya corona, wizara imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha wanafunzi wamemaliza silibasi bila matatizo yoyote.

Kaunti hiyo ina jumla ya watahiniwa 26, 298 katika vituo 411.

Kati ya watahimiwa hao, 12, 644 ni wavulana huku 13, 654 wakiwa wasichana.

Katika Kaunti ya Isiolo, jumla ya watahiniwa 1,701 wanafanya mitihani yao katika vituo 31.

Kamishna wa kaunti hiyo, Geoffrey Omoding, alitoa hakikisho kuwa serikali itatuma vikosi vya kutosha katika maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama ili kuhakikisha watahiniwa wanafanya mtihani wao bila matatizo yoyote.

Katika Kaunti ya Kakamega, walimu wakuu walielezea matumaini yao kwamba matokeo ya mtihani huo yatakuwa bora ikilinganishwa na miaka ya hapo nyuma.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Kakamega School, Bw Gerald Orina, amesema kuwa watahiniwa wote 480 ambao walijisajili kufanya mtihani katika shule hiyo waliuanza bila tatizo lolote.

Taarifa za Okong’o Oduya, David Muchui, Reginah Kinogu, Alex Njeru, Waweru Wairimu na Shaban Makokha

You can share this post!

James Nandi: Afisa wa serikali aliye kielelezo bora kwa raia

Urithi wa Joho wazua taharuki

T L