Makala

Anavyopiga jeki kina mama kuendeleza ufugaji kuku    

March 17th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

DKT Teresia Wairimu amezuru mataifa tofauti ndani na nje ya Bara Afrika lengo likiwa kuona yanavyofanya ufugaji hususan wa kuku.

Safari hizo zimetokana na kazi aliyokuwa akifanya awali; kuhudumia wakulima.

Akilinganisha Kenya na baadhi ya nchi alizozuru, anakiri ufugaji kuku una faida ila hapa nchini tunahitaji kuwa wabunifu.

“Ndio, biashara ya kuku ina hela japo tunapaswa kubaini mahali pa kukaza nati kwa kukumbatia bunifu za kisasa,” anasema.

Dkt Wairimu ni mwasisi wa Jolly Footprints Ltd, kampuni inayoangua vifaranga.

Mwasisi Jolly Footprints Ltd, Dkt Teresia Wairimu akilisha vifaranga katika mradi wake ulioko Kajiado. PICHA|SAMMY WAWERU

Si vifaranga wa kawaida, ila ni wa kuku wa kienyeji walioboreshwa kama vile Kari, Kuroiler, Rainbow rooster, Sasso na Kenbro.

Kulingana na mtaalamu huyu, wafugaji wanapaswa kubadilisha mbinu wanazotumia kuendeleza biashara ili kuwahi soko lenye ushindani mkuu.

Dkt Wairimu anasema, isiwe ni kuku wa kutaga mayai na kuyasukuma yote sokoni.

Na si ufugaji wa aina yoyote ile ya kuku, bali kuku wenye thamani kama wa kienyeji halisi na walioboreshwa.

“Kimsingi, mayai unapoyaongeza thamani kuwa vifaranga mapato yanaongeza,” anasema.

Dkt Teresia Wairimu akionyesha vifaranga anaofuga katika mradi wake Nkoroi Kaskazini. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni kutokana na uzoefu aliopata kuhudumia wakulima maeneo mbalimbali nchini, Dkt Wairimu alivumbua gapu hiyo.

Isitoshe, mfugaji huyu hodari anasisitizia umuhimu kutambua wateja (niche market).

Katika mazingira tulivu ya Nkoroi Kaskazini, Kaunti ya Kajiado, ndiko iliko Jolly Footprints Ltd.

Kampuni hiyo inaangua vifaranga, Dkt Wairimu akifichua kwamba anahudumu na makundi ya kina mama na vijana mashambani.

Dkt Teresia Wairimu kupitia mradi wake wa kuku ulioko Nkoroi Kaskazini, Kajiado hupiga jeki kina mama na vijana. PICHA|SAMMY WAWERU

Kufanikisha sekta ya kuku, kulenga vijana na kina mama anaamini ndio msingi.

“Mambo yanabadilika, wanawake sasa wameanza kumiliki biashara za kilimo na mojawapo ya mbinu kuinua jamii ni kulenga kina mama kwa kuwahamasisha waingilie ufugaji kuku,” anaelezea, akikumbuka jinsi alivyoshuhudia kwenye huduma zake kina mama mashinani wakitegemea ufugaji kuku kukithi familia mahitaji muhimu ya kimsingi.

Hata ingawa mradi wa Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS) kupitia mpango wa United States Agency for International Development (USAID) unaolenga kupiga jeki wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula nchini ulikunja jamvi 2023, Dkt Wairimu anadokeza kwamba ulimwezesha kufikia wafugaji wasiopungua 6, 000.

Vifaranga wa kuku walioboreshwa anaoangua Dkt Teresia Wairimu katika mradi wake Kajiado. PICHA|SAMMY WAWERU

Wengi ni kina mama na vijana.

Kitaifa, Afisa Mkuu Mtendaji huyu wa Jolly Footprints Ltd anasema anahudumu na zaidi ya wakulima 10, 000.

“Kila mwezi, huwasambazia vifaranga kati ya 15, 000 hadi 20, 000,” akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano ya kipekee.

Kuhamasisha na kuvutia wafugaji, kwa wanaojiunga na mradi wake huwauzia vifaranga kwa ‘bei ya punguzo’, mfano, mkulima anaponunua 40 anaongezewa 10 zaidi.

Isitoshe, hutoa mafunzo jinsi ya kufanya ufugaji wa kuku kitaalamu; kuanzia matunzo ya vifaranga, malisho hadi wanapokomaa kuanza kutaga.