Makala

Anavyounda chakula cha mifugo kwa gharama ya chini

January 10th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

JOSEPH Kamau, ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Murang’a ambaye licha ya ugumu unaozingira sekta ya ufugaji nchini anajikaza kuhakikisha kiungo hicho cha kinywaji kinapatikana.

Kamau, maarufu kama JD katika Kijiji Kabucii, Kangema, aliingilia ufugaji wa ng’ombe 2016 kama mojawapo ya mbinu kujipa pato la ziada.

Alikuwa afisa wa masuala ya mifugo katika Wizara ya Kilimo na Ufugaji, ambapo alistaafu 2020.

Anadokeza kwamba alianza na ng’ombe mmoja aliyemnunua Sh35, 000 kisha baadaye akaongezea mwingine, na anahoji ikiwa kuna wakati mgumu katika ufugaji uite baada ya Kenya kukumbwa na janga la Covid-19 mwaka 2020.

“Chakula cha mifugo cha madukani kinauzwa mithili ya dhahabu,” Kamau anasikitika.

Mfugaji Joseph Kamau akiwa kwenye ‘kituo’ chake cha kusaga nyasi maalum za ng’ombe. PICHA|SAMMY WAWERU

Changamoto hiyo hasa inatokana na uhaba wa malighafi, jambo ambalo ni kero ya kimataifa, ikichochewa zaidi na VAT na ada za juu zinazotozwa malighafi na madini nchini.

Isitoshe, chakula kingi kinachouzwa masokoni Kamau analalamikia kutoafikia ubora wa bidhaa akikumbuka alipoanza ufugaji jinsi ng’ombe wake wasingepitisha wastani wa lita mbili kila siku.

Hata hivyo, mtaalamu huyu mekumbatia mfumo wa kujiundia chakula.

Nimekodi vipande kadhaa vya mashamba ambapo hukuza nyasi kama vile ya mabingbingo (Napier Grass) na Desmodium, Kamau anaelezea.

Nyasi zinazompa tabasamu zaidi ni zile za kisasa Super Napier maarufu kama Pakchong.

“Manufaa yake kiafya kwa mifugo ni mara tatu ya nyasi za kawaida,” anasifia, akidokeza kwamba zimemfanikisha kupandisha kiwango cha uzalishaji maziwa kutoka lita mbili hadi kumi kwa siku kila ng’ombe.

Mfugaji huyu ana jumla ya ng’ombe watano, wawili wakiwa ni ndama.

Aidha, anakama watatu.

Picha 6: Joseph Kamau akielezea kuhusu uundaji wa silage. PICHA|SAMMY WAWERU

Ana chaff cutter ya kusaga malisho, ambayo huchanganya na virutubisho kama vile Maize Germ, wheat pollard, cotton seed cakegroundnut seed cake na sunflower seedcake.

“Ni muhimu kuwa na fomula ya kuchanganya virutubisho na madini faafu kwa mifugo,” anahimiza.

Mfugaji huyu hodari, vilevile huunda silage anayosema humsaidia sana kiangazi kinapobisha hodi.

“Januari hadi mwezi Machi, na Agosti hadi Oktoba aghalabu huwa na uhaba wa malisho kwa sababu ya kiangazi, na silage ni hifadhi ya nyakati ngumu kama hizo,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano kwenye mradi wake Kangema.

Kiangazi na ukame ni kati ya athari zinazochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) likiorodhesha Kenya kama kati ya nchi zilizolemewa pakubwa Upembe wa Afrika.

Kamau alisema hununua kiwango kidogo tu cha chakula cha madukani, akikadiria mkondo aliochukua kujiundia malisho unampunguzia karibu asilimia 30 ya gharama.

Kando na kuzalisha maziwa, Joseph Kamau pia anazalisha kawi – biogas inayotumika kufanya mapishi nyumbani kwake. PICHA|SAMMY WAWERU

Mradi wake wa ng’ombe wa maziwa umekalia kipande cha ardhi cha futi 20 kwa 20, zizi likiwa la ghorofa, paa akilitumia kuhifadhi chakula.

Cha kuridhisha zaidi, mfugaji huyu wa haiba yake anazalisha kawi – gesi (biogas) kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe, inayotumika kufanya mapishi nyumbani kwake.

Anapigia upatu teknolojia hiyo, akisema ni mojawapo ya mbinu kupunguza kuenea kwa gesi hatari aina ya Methane.

Yote tisa, soko lake likiwa baadhi ya kampuni kuongeza maziwa thamani na kuyasindika, analalamikia bei kuwa duni akifichua kwamba lita moja hununuliwa chini ya Sh43.

Shukran kwa Gavana wa Murang’a, Dkt Irungu Kang’ata, anayesema anaendeleza mpango kuwapa wakulima bonasi ya Sh3 kwa kila lita.

Hata hivyo, mradi huo unawafaa wafugaji wanaouza maziwa kupitia vyama vya ushirika vilivyosajiliwa.

Chini ya mradi wake, Kabucii Dairy Farm, Kamau anafuga ng’ombe aina ya Jersey.

Joseph Kamau akiwa na mkewe ambaye ni mwalimu, kwenye jiko linalotumia kawi ya biogas. PICHA|SAMMY WAWERU