Habari Mseto

Anayetakiwa Afrika Kusini kwa utekaji nyara aachiliwa huru

April 30th, 2020 2 min read

 

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA wa familia ya aliyekuwa mlanguzi wa dawa za kulevya marehemu Ibrahim Akasha, Haisam Majid Ajip anatakiwa na serikali ya Afrika Kusini kushtakiwa kwa makosa ya utekaji nyara wa msichana mwenye umri wa miaka 15.

Ajip aliachiliwa na kukamatwa tena na kupelekwaa kituo cha Polisi cha Gigiri.

“Ajip amepelekwa kituo cha Gigiri,” wakili wake Bw Mbiyu Kamau aliambia ‘Taifa Leo’ kwa simu akiwa katika kituo hicho cha Polisi.

Kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 mshukiwa huyo hawezi kusafirishwa kutoka Kenya hadi Afrika Kusini.

Hata hivyo, mshukiwa huyo alikamatwa punde tu alipotoka mbele ya hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) aliomba Bw Ochoi amwachilie mshukiwa huyo kwa vile amekuwa katika kizuizi cha polisi kwa siku 21.

“Ombi hili la kumwachilia mshukiwa huyu sio kusema hatachukuliwa hatua ya kisheria kulingana na madai kwamba amemteka nyara msichana wa umri mdogo,” Bw Ochoi alielezwa na kiongozi wa mashtaka.

Bw Ajip aliwakilishwa na mawakili Mbiyu Kamau na Mbugua Mureithi.

Mabw Mureithi hawakupinga ombi la DPP na kuongeza endapo anatakiwa na polisi atashirikiana nao kwa uchunguzi zaidi.

Lakini wakili wa familia ya msichana huyo Dkt John Khaminwa imeomba mahakama iamuru DPP afichue ushahidi aliopata katika kesi hiyo ndipo hatua kali zichukuliwe.

Hata hivyo, kiongozi wa mashtaka aliomba mahakama imwachilie Ajip kwanza ndipo polisi waendelee na uchunguzi zaidi kwa lengo la “kumshtaki.”

Akiruhusu ombi la DPP, hakimu alisema mshukiwa huyo alitiwa nguvuni Aprili 9, 2020, na amekuwa korokoroni.

Alisema DPP ameeleza kuwa hajakamilisha uchunguzi.

Hakimu alielezwa mshukiwa huyo alipitia nchini Tanzania kutoka Afrika Kusini akiwa na mlalamishi.

DPP alisema msichana huyo anazuiliwa katika idara ya watoto.

DPP alisema ombi litawasilishwa katika mahakama ya watoto na kuomba msichana huyo apatiwe idhini arudishwe Afrika Kusini.

“Sitasema chochote kuhusu msichana huyo kwa sasa. DPP awasilishe kesi katika mahakama ya watoto,” alisema Bw Ochoi.

DPP alisema mshukiwa huyo atafikishwa kortini wiki ijayo.

Hakimu aliamuru afisi ya DPP iwasiliane na Dkt Khaminwa kuhusu taarifa za uchunguzi katika kisa hicho.