Habari Mseto

Aliyetarajia kuingia kidato cha kwanza auawa na stima

December 5th, 2019 1 min read

Na George Munene

MWANAFUNZI aliyefanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka huu na aliyetarajiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza amefariki, baada ya kupigwa na stima katika kijiji cha Thumari, Kaunti ya Kirinyaga.

Mwathiriwa, aliyetambuliwa kama Dominic Githinji, 15, alifariki jana baada ya kugusa waya ya stima kimakosa katika chumba chake cha kulala.

Mwili wake uligunduliwa na jirani yake, ambaye baadaye aliwafahamisha wenzake.Nyanyake mvulana huyo, Bi Edith Mugo, alieleza jinsi alishangazwa na habari kuhusu tukio hilo.

“Nilikuwa nikikaa pamoja na mjukuu wangu. Alifanya mtihani wa KCPE mwaka huu na kupata matokeo yake majuzi. Nusura nizimie niliposikia kuhusu yaliyomfika,” akasema, alipowahutubia wanahabari.

“Mwanzoni, sikuamini mjukuu wangu amefariki hadi nilipouona mwili wake,” akaongeza.Naibu Chifu katika eneo hilo Bi Josephine Gitari alisema kwamba alikuwa akielekea kazini alipofahamishwa kuhusu kisa hicho.

“Baada ya kufahamishwa, nilielekea hapo kwa haraka, ambapo niliwakuta wakazi wenye hofu wakiwa wamekusanyika,” akasema.

Mkuu wa Polisi katika eneo la Kirinyaga Mashariki Bw Anthony Wanjuu alisema kwamba uchunguzi umeanza.