UFUGAJI: Anazingatia mbinu bora kuwafuga ng’ombe wake

UFUGAJI: Anazingatia mbinu bora kuwafuga ng’ombe wake

NA SAMMY WAWERU

MRADI wa ng’ombe wa maziwa wa Edwin Njuguna, anaouendelezea katika Kaunti ya Murang’a ni wenye manufaa tele.

Ukiwa katika kijiji cha Pundamilia, Maragua, unaendelea kumvunia sifa kufuatia mchango wake mkuu katika mtandao wa uzalishaji maziwa. Njuguna, 35, anasema alianza na ufugaji nguruwe ambapo pia alijumuisha ng’ombe japo wa maziwa ya familia yake.

“Nguruwe walikuwa wa biashara,” asema.

Ng’ombe, alinunua watano wakimgharimu jumla ya Sh250,000.

Wawili aidha ndio walikuwa wanazalisha maziwa, na kulingana na Njuguna kiwango alichopata kilizidi kwa kiasi kikubwa walichohitaji familia yake.

“Mmoja alikuwa akizalisha lita 30 na mwingine 10 kwa siku, ilhali familia ilihitaji lita tatu pekee,” asema.

“Nilipata msambazaji Nairobi wa yaliyosalia, na mwezi mmoja baadaye malipo yalinishawishi kuchukua hatua nyingine,” anakumbuka.

Njuguna, baba wa watoto watatu, anasema mahesabu aliyofanya yaliashiria faida tupu.

Ulikuwa wakati ambao biashara ya nguruwe ilikuwa inampiga chenga, kwa kile anachosema kama gharama ya malisho kumlemea.

Kufuatia maamuzi ya Njuguna, anayotaja kuwa ya busara, yaliyofuata yamekuwa historia ya ufanisi.

Katika shamba lake lenye ukubwa wa ekari mbili, robo ni mradi wa ng’ombe wa maziwa.

Mazizi, yamejengwa kwa mbao, mabati na kukorogewa saruji, akifichua yalimgharimu karibu Sh2.4 milioni.

Yamegawanywa kulingana na umri wa ng’ombe na hali.

Yana sehemu tatu za kukama maziwa, makazi tisa ya ndama wenye umri kuanzia siku moja hadi miezi mitatu.

Vilevile, ana vipande vingine 22 vya ng’ombe ambao hawajazaa.

Mradi wake pia, una sehemu ya ng’ombe kujifungua.

“Hali kadhalika, wenye matatizo mbalimbali na wanaougua nimewajengea eneo maalum kuwahudumia na matibabu,” aelezea.

Mazizi yote, yana vifaa vya kuwatilia lishe, na kukumbatia mfumo wa mifereji kukata kiu cha maji, na sehemu za mapumziko zenye magodoro.

Mfugaji huyo mwenye Stashahada ya Juu katika Masuala ya Stima, kwa sasa ana ng’ombe 22 wanaozalisha maziwa.

Anaiambia Akilimali, ng’ombe anayezalisha kiwango cha chini ni lita 13 kwa siku, cha juu kikiwa 50.

“Bei yangu ni ya jumla, na inachezea kati ya Sh42 – 50 kwa lita,” asema, akidokeza mteja wake mkuu ni Loyalty Dairies.

Kando na biashara ya maziwa, ana soko la ng’ambo la ng’ombe wake akitaja nchi ya Comoros miongoni mwa wanunuzi.

Gharama ya juu ya chakula cha madukani, ndio kikwazo kikuu sawa na changamoto zinazokumba wafugaji wengine.

Njuguna amekodi mashamba kadha kukuza mahindi, mimea anayoitumia kutengeneza silage.

Pia, hulima viazi vikuu vitamu akisema majani yake na viazi vyenyewe, huwa na virutubisho tele vinavyosaidia ng’ombe kuzalisha maziwa kwa wingi. Kadhalika, amekuza nyasi maalum aina ya Lucerne, zile za mabingobingo na hay akinunua kutoka kwa wakuzaji.

  • Tags

You can share this post!

Re-Union FC yaweka mikakati kurejesha fahari kama zamani

Ubinafsi watajwa kiini cha viongozi kuhama kila mara

T L