Michezo

Ancelotti na wachezaji wake wakubali kukatwa mishahara

June 12th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WACHEZAJI wa Everton wamehiari kunyofolewa asilimia 50 ya mishahara yao kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo katika juhudi za kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kukabiliana na janga la corona.

Kocha Carlo Ancelotti pamoja na benchi yake nzima ya kiufundi wamekuwa wakikatwa mishahara yao kwa hadi asilimia 30 tangu kuripotiwa kwa virusi vya corona.

Denise Barrett-Baxendale ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Everton, amewashukuru pakubwa wachezaji na maafisa wa benchi ya kiufundi kwa hatua yao hiyo ambayo kwa mujibu wake, ni dhihirisho la kiwango kikubwa cha kujitolea.

Hadi kufikia sasa, mashabiki wa Everton wamechanga kima cha Sh56 milioni walizokuwa watumie kwa minajili ya mahudhurio ya mechi zilizosalia msimu huu ili kusaidia familia zilizoathiriwa pakubwa na homa corona.

Everton owner Farhad Moshiri and chairman Bill Kenwright have matched the figure, added Barrett-Baxendale.

Mmiliki wa Everton, Farhad Moshiri, mwenyekiti Bill Kenwright na Barrett-Baxendale wametoa pia kila mmoja kiasi sawa na hicho cha mchango kwa minajili ya hazina maalum ya kuwapiga jeki vibarua na wafanyakazi ambao wameathiriwa na corona.

Everton ambao kwa sasa wamechangisha zaidi ya Sh112 milioni wamepangiwa kurejelea kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa gozi la Merseyside litakalowakutanisha na Liverpool uwanjani Goodison Park mnamo Juni 21.

Liverpool ambao wanafukuzia ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 huenda wakalitwaa ubingwa huo katika mchuano huo iwapo washindani wao wakuu, Manchester City watazidiwa maarifa na Arsenal mnamo Juni 17 ugani Etihad.