Michezo

ANDAZI MOTO: Rodriquez awaniwa

May 24th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

LIVERPOOL, Arsenal na Manchester United zinamezea mate winga James Rodriguez, ambaye ripoti zinadai ameamua hana haja kuendelea kuchezea miamba wa Ujerumani Bayern Munich.

Klabu hizi kutoka nchini Uingereza, hata hivyo, zinakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa miamba Juventus (Italia) na mabwanyenye Paris Saint-Germain (Ufaransa), ambao wanasemekana wanafuatilia kwa makini hali yake katika klabu ya Bayern.

Ripoti zinadai kwamba Rodriguez analenga kuondoka Bayern mwisho wa msimu huu.

Raia huyu wa Colombia alitua Bayern mwaka 2017 kuichezea miaka miwili kwa mkopo kutoka Real Madrid ambako alikosa kuridhisha.

Licha ya kuanzishwa katika mechi nyingi kuliko ilivyokuwa nchini Uhispania, Rodriguez ameshindwa kutulia kabisa uwanjani Allianz Arena.

Amechangia mabao 15 na kumega pasi 20 zilizozalisha mabao katika mechi 67 katika mashindano yote na kusaidia Bayern kutwaa mataji ya Ligi Kuu katika misimu hiyo miwili.

Wafalme hawa wa Ujerumani walikuwa na fursa ya kumnunua kabisa kwa Sh4.7 bilioni, lakini kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Ujerumani, Rodriguez hayuko makini kuendelea kuwa nao.

Rodriguez anataka kurejea Real Madrid anakopatikana wakala wake, Jorge Mendes, ambaye ataamua atakoelekea.

Inatarajiwa kwamba Rodriguez ataondoka Madrid wakati huu kocha Mfaransa Zinedine Zidane anapanga kufanyia kikosi chake mabadiliko makubwa katika kipindi kirefu cha uhamisho.

Mwanasoka bora wa mwaka 1998, 2000 na 2003, Zidane haoni kiungo huyo mbunifu akiwa katika mipango yake ya muda mrefu, na hili limevutia timu kutoka Ligi Kuu ya Uingereza.

Klabu za Uingereza zamtaka sana

Sasa, inasemekana kwamba Liverpool, Manchester United na Arsenal zote zinataka kumleta nchini Uingereza, huku mabingwa wapya wa Italia Juventus na wafalme wa Ufaransa, Paris Saint-Germain, wakifuatilia kwa karibu sana hali yake.

Real iko tayari kuuza Rodriguez ili kuimarisha kitita chake cha kujitosa sokoni kabla ya kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake.

Kiungo mbunifu wa Chelsea, Eden Hazard anasalia juu ya orodha ya wachezaji Real inataka, huku Zidane pia akithibitisha kwamba anatamani kupata huduma za kiungo wa United, Paul Pogba.

Habari zaidi kutoka uwanjani Old Trafford zinadai kwamba United pia inataka kusajili kiungo Mfaransa Adrien Rabiot, ambaye anatarajiwa kuondoka Paris Saint-Germain baada ya kandarasi yake kukatika mwisho wa msimu huu.

United inasemekana pia imeimarisha ofa ya Sh1.5 bilioni kila mwaka iliyowasilisha kwa beki wa Ajax, Matthijs de Ligt na imejawa na matumaini mchezaji huyu Mholanzi mwenye umri wa miaka 19 atajiunga nayo.

Wakati huo huo, beki Mwitaliano Matteo Darmian, 29, mshambuliaji Mbelgiji Romelu Lukaku,26, kiungo Mhispania Juan Mata, 31, na beki kutoka Argentina Marcos Rojo, 29, wanaaminika watahama United katika kipindi hiki cha uhamisho.

Tetesi zinasema kwamba Inter Milan itapatia United Sh3.8 bilioni pamoja na winga wa Croatia Ivan Perisic, 30, kupata huduma za Lukaku.

Ripoti zinadai kwamba Lukaku amekuwa na wasiwasi kwamba Sh8.9 bilioni ambazo United inaitisha ili imruhusu aondoke huenda ikavuruga uhamisho wake hadi Inter, ambayo iko tayari kumchukua kwa Sh6.4 bilioni.

Nayo Arsenal inapanga kufukuzia winga Ryan Fraser, 25, baada ya fainali ya Ligi ya Uropa dhidi ya Chelsea hapo Mei 29.

Waajiri wake Bournemouth watamruhusu aondoke kwa Sh3.8 bilioni. Arsenal pia inaaminika kuwa katika orodha ya timu zinazotafuta huduma za mshambuliaji Muingereza Danny Loader, 18, kutoka klabu ya Reading.