Michezo

ANENE: Hongera Cecafa kumpa Kerr wembe alioulilia

July 16th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Naikaribisha hatua ya kijasiri iliyochukuliwa na Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kupiga marufuku kocha mkuu wa Gor Mahia Dylan Kerr miaka miwili kwa kurushia marefa cheche za matusi bila kukoma.

Marufuku hii ilistahili kutolewa mapema. Ingefanywa nchini Kenya na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ama kampuni inayoendesha Ligi Kuu nchini Kenya (KPL) pengine Muingereza huyu angekuwa amejifunza kabla ya marufuku ya Cecafa ambayo inamzuia kuongoza klabu ama timu yoyote ya taifa itakayoshiriki mashindano ya Cecafa katika kipindi hicho.

Ilikuwa muda tu kabla ya Kerr apokee adhabu hiyo.

Si mara moja ama mbili kocha huyu mwenye umri wa miaka 51 amesikika akitusi marefa katika mashindano mbalimbali ya Kenya ikiwemo Ligi Kuu. Pia ni mara kadhaa ametoka katika kisanduku cha makocha wakati wa mechi na pia kusikika akiongelesha wasimamizi wa mechi vibaya licha ya kuonywa.

Itakukumbwa kwamba mwaka 2017 alijipata pabaya kwa tabia hii. Hata hivyo, inaonekana faini ya Sh2, 500 pekee kwa kuingia uwanjani na pia kuvunja kiti kimoja cha plastiki uwanjani Thika wakati Gor ikichuana na Mathare United haikutosha kumuonyesha anavuka mipaka.

Kabla ya hapo, KPL ilikuwa imemuonya alipoingia uwanjani akilalamikia bao la Gor ambalo halikuhesabika dhidi ya Sofapaka mnamo Septemba 27, 2017.

Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba, licha ya kuwa kocha mzuri na ambaye kazi yake Gor haiwezi kutiliwa shaka tangu ajiunge nayo Julai mwaka 2017, Kerr amekuwa na kiburi cha kuendeleza tabia hii inayoenda kinyume na maadili ya michezo.

Adhabu ya Cecafa inafaa kuwa funzo sio tu kwa Kerr, bali pia makocha wengine nchini Kenya. KPL na FKF zinafaa kuiga Cecafa katika utoaji wa adhabu ndiposa makocha wajifunze kudumisha nidhamu.

Kerr alipokea marufuku jijini Dar es Salaam nchini Tanzania akiongoza Gor katika mashindano ya Kagame Cup ambayo timu yake ilimaliza katika nafasi ya tatu. Gor haikukwepa marufuku sawa na hiyo baada ya wachezaji wake kukataa kujitokeza katika hafla ya kupewa medali. Naipongeza Cecafa kwa kuchukua msimamo huu. Jinsi Cecafa ilivyosema, klabu yoyote haifai kudharau sheria kwa “kuhisi haiwezi kuguswa.”