Michezo

Angalia orodha ya Ballon d’Or ujue gani kali kati ya La Liga na EPL

October 15th, 2018 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

MWANZONI mwa wiki iliyopita, nyota wa Juventus Cristiano Ronaldo na mfumaji matata wa Manchester City Sergio Aguero, walikuwa miongoni mwa wachezaji walioteuliwa kuwania tuzo ya Ballon d’Or mwaka huu.

Kuna pia wachezaji wa Chelsea, Eden Hazard na N’Golo Kante; na fowadi matata mzawa wa Wales, Gareth Bale anayechezea Real Madrid katika orodha hiyo ya kuwania taji hilo ambalo hutolewa kwa Mchezaji Bora zaidi duniani.

Waandalizi wa tuzo hiyo walikuwa wakiwatangaza wawaniaji wa mwaka huu kwa mafungu hadi wakafikia wachezaji 30 wanaounga orodha fupi ya awali kabisa.

Katika orodha hiyo ya 30-bora, kunao wachezaji 14 wanaosakata soka katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na 11 katika vikosi vinavyowania Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Ligi Kuu ya Italia (Serie A) inawakilishwa na wachezaji wawili pekee huku Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ikiwa na wawakilishi watatu.

Miongoni mwa Ligi Kuu tano maarufu zaidi katika soka ya bara Ulaya, ni Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ndiyo ilikosa mwakilishi.

Ballon d’Or ni tuzo maarufu ambayo imekuwa ikitolewa tangu 1956; na sherehe ya kumtangaza mshindi mwaka huu itafanyika jijini Paris, Ufaransa mnamo Desemba 3. Mchezaji Bora wa kike duniani pia atatunukiwa kwa mara ya kwanza mwaka huu. Mshambuliaji wa Ureno Cristiano Ronaldo, aliyehamia Juventus kutoka Real Madrid msimu huu ndiye aliyetawazwa mfalme wa tuzo hiyo mwaka jana.

Nyota wa Chelsea, Eden Hazard aliwahi kusema kwamba anawazia kuhusu uwezekano wa kuhamia Real Madrid mwaka ujao kwa kuwa tamanio lake kuu maishani limekuwa kuvaa jezi za kikosi hicho. Isistoshe, alikariri kuwa Real ni miongoni mwa vikosi vinavyoshiriki ligi bora zaidi duniani.

Huku mafanikio ya klabu za La Liga yakipania kutusadikisha kwamba soka ya Uhispania ndiyo inayosheheni utajiri mkubwa zaidi wa talanta na vipaji, nahisi kuwa ubora wa EPL siku hizi umo tu katika wingi wa fedha zinazomwagwa sokoni kwa minajili ya kusajili wachezaji wapya na upeperushaji wa moja kwa moja wa mechi za kivumbi hicho.

Kinachowachochea mashabiki wengi kuamini kwamba La Liga ni bora zaidi kuliko EPL ni ubabe wa watani wakuu wa soka ya Uhispania; yaani Real, Barcelona na Atletico.

Katika orodha ya wawaniaji wa mwaka huu, soka ya Uingereza inawakilishwa na Sergio Aguero (Man-City), Alisson Becker (Liverpool), Kevin de Bruyne (Man-City), Roberto Firmino (Liverpool), Eden Hazard (Chelsea), Harry Kane (Tottenham), N’Golo Kante (Chelsea), Hugo Lloris (Tottenham), Sadio Mane (Liverpool), Paul Pogba (Man-United) na Mohamed Salah (Liverpool).

Wawakilishi wa soka ya Uhispania ni Gareth Bale (Real), Karim Benzema (Real), Thibaut Courtois (Real), Diego Godin (Atletico), Antoine Griezmann (Atletico), Isco (Real), Marcelo (Real), Luka Modric (Real), Ivan Rakitic (Barcelona), Sergio Ramos (Real), Jan Oblak (Atletico), Lionel Messi (Barcelona), Luis Suarez (Barcelona) na Raphael Varane (Real).

Ronaldo na Mario Mandzukic ambao wanavalia jezi za Juventus wanawakilisha soka ya Italia huku wavamizi matata wa PSG Edinson Cavani, Kylian Mbappe na Neymar wakiwakilisha soka ya Ufaransa.