ANGELA CHEGE: Analenga kumpiku Anne Kansiime

ANGELA CHEGE: Analenga kumpiku Anne Kansiime

Na JOHN KIMWERE

PENYE nia pana njia. Ndivyo wahenga walivyologa, tangia zama zile baada ya kupasua hilo mpaka sasa, msemo huo ungali na mashiko siyo haba miongoni mwa jamii kwa jumla.

Angela Chege ni kati ya wasanii chipukizi wanaojiwekea matamanio ya kutinga upeo wa kimataaifa miaka ijayo. Hata hivyo kwa jina la msimbo anafahamika kama Angie The Twerker.

Dada huyu ni miongoni mwa wasanii wanaokuja wanaopania kujituma kiume katika masuala ya vichekesho na maigizo hapa nchini. Pia ni mratibu wa sherehe (MC) na muuza wa bidhaa mbali mbali (Marketer).

Kando na masuala ya uigizaji kipusa huyu huandaa kipindi kiitwacho ‘Chit Chat’ ambacho hupeperushwa kupitia Ebru TV kila Jumamosi, ambapo huwa wanazungumzia kuhusu hoja tofauti kuhusu maisha kwa vijana.

”Bila shaka nilianza masuala ya uigizaji nikisoma Shule ya Msingi lakini ukweli wa mambo sikufahamu kama ingeibuka kuwa kati ya taaluma zangu. Binafsi ninaelewa sijapiga hatua kubwa katika tasnia ya uigizaji lakini ninaendelea kujijenga,” anasema na kuongeza kuwa anatosha mboga kufanya vizuri ndani ya miaka ijayo.

Katika mpango mzima dada huyu mwenye umri wa miaka 23 amepania kujibiidisha kiume kuhakikisha ameiva na kumpiku mchekeshaji mahiri mzawa wa Uganda, Anne Kansiime.

Kisura huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa na kupata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga tofauti tangia aanze kushiriki masuala ya maigizo mwaka 2015.

Msichana huyu ameshiriki vipindi mbali mbali kama Hulla Baloo (Maisha Magic East). Pia ameshiriki shoo ya Hello Mr Right ( Star Times), Perfect Match (Ebru TV) na Dondoo za DJ Shiti (KTN Home).

Kwenye juhudi za kuonesha talanta yake katika uigizaji amebahatika kufanya kazi na wasanii kama Victor Naman, Yy Comedian na DJ Shiti. Anasema amefanikiwa kufanya kazi na Gendy Prodution ya Nakuru na Naxvegaz Theatre. Msichana huyu mwenye tabasamu ya kuvutia anasema anatamani sana kufanya kazi na msanii, Kansiime.

Anatoa wito kwa wasanii wa Kenya wawe wabunifu, umoja na kusaidiana ili kujenga sekta ya maigizo na kutengeneza nafasi za ajira. Hata hivyo anaponda baadhi ya wenzake wa humu nchini na kusema hawapendi kujituma kwa kazi zao.

”Sina shaka kutaja kuwa wasanii wenzangu wafahamu jukwaa la maaigizo hakuna mteremko lazima wajitume kiume kutafuta ajira hasa kwa kushiriki majaribio,” akasema na kuongeza kuwa serikali inastahili kutenga fedha za kufadhili sekta ya maigizo ili kusaidia wasanii wanaoibukia.

CHANGAMOTO

Anashikilia kuwa katika sekta ya maigizo wanapitia pandashuka nyingi tu ikiwamo kukosa fedha za kugharamia miradi yao. ”Ningependa kushauri wanawake wenzangu kuwa ni muhimu tuwe wabunifu ili kujihepusha dhidi ya changamoto za kukosa ajira. Kiukweli taifa hili lina waigizaji wengi tu ambao wametunukiwa kipaji cha uigizaji lakini nafasi za ajira ni chache,” akasema.

You can share this post!

Tulianza vibaya lakini tuna matumaini tutamaliza vyema...

JULIUS MWANZIA: Msanii chipukizi wa injili, produsa mtajika